Erick Omondi amtaja Salasya kama msaliti namba moja

Erick Omondi amemtaja Salasya kama msaliti anayenunuliwa na serikali kwa pesa kidogo hii ni baada ya Erick kudai kuwa Salasya hapiganii wakenya.

Muhtasari

•Erick Omondi amemtaja Salasya kama msaliti namba moja kati ya wabunge wote kwa kukosa kuwapigania wakenya.

•Erick amemwomba Salasya  avuke mpaka ili awe mstari wa mbele kuwapigania wakenya badala ya kununuliwa na serikali.

Eric Omondi
Eric Omondi
Image: Facebook

Erick Omondi pamoja na mbunge wa Mumias mashariki Peter Salasya wamezidi kutupiana cheche za maneno kupitia mtandao. 

Majibizano haya yalijiri baada ya Erick Omondi kuongoza maandamano mbele ya bunge siku chache zilizopita.

Mchekeshaji na muunda maudhui ya kidijitali,Erick Omondi aliongoza maandamano pamoja na akina  mama mboga huku wakirusha mboga aina ya sukuma, mbele ya bunge kabla ya kukamatwa na maafisa wa polisi,jambo ambalo lilileta utata na majibizano kupitia mitandao ya kijamii kati ya mbunge Peter Salasya na Erick Omondi.

Peter Salasya alionyesha kukerwa baada ya Erick Omondi kuwaita wabunge wasaliti  wakati wa maandamano huku akidai kuwa lazima Erick Omondi afikirie kabla ya kuongea.

"….toa vipindi kwa vipindi hivi tunazijua …ikifika kwa vipindi vya siasa uliza." Peter Salasya aliandika kwa ukurasa wake wa X almaarufu twitter.

 Eric aliendelea kumtaja Salasya kama msaliti nambari moja kwa kutounga mkono maandamano yake.Hii ni baada ya kuona chapisho la  Salasya kwenye ukurasa wake.

Kwenye mahojiano na waandishi wa kidijitali ,Erick alifichua  kwamba Salasya amenunuliwa na serikali na kwamba anashirikiana nao sasa baada ya kufurahia anasa za serikali.

"Anafurahia anasa za serikali. Yeye ndio msaliti namba 1. He’s been bought. Yuko kitandani na serikali..." Erick alisema.

Eric aliongeza kuwa Salasya amekuwa akipiga picha na rais pamoja na  naibu rais  kwenye ziara wakielekea Marekani huku akidai kuwa amelipwa ilihali Salasya amesahau ametoka kwa familia ya wastani.

"Erick Omondi unafahamu ni viongozi wangapi kutoka Nyanza wamekutana na rais na hata kufikia hatua ya kuandamana na rais hadi Marekani? Wajinga waliisha Kenya na next time ukisahau kumwaga omena bungeni na kumwaga sukuma tu vile ulivyofanya,sitakutoa jela tena..." Salasya aliandika kwa ukurusa wake wa Facebook.

Vilevile Salasya amesema kuwa Erick anatafuta tu umaarufu na wala hayuko mstari wa mbele wa kuwasaidia  wakenya.

 

Wawili hao  aidha bado hawajasuluhisha malumbano yao. Eric aliahidi kuendelea kupigana dhidi ya mswada  wa fedha wa 2024,akitaja kuwa wakenya watateseka baada ya kupitishwa  kwa mswada huo.