Familia ya Njambi Koikai yaeleza sababu ya kuafikia kumzika katika makaburi ya Lang’ata

Mshabiki huyo mkuu wa Reggae aliyefariki mapema wiki jana atazikwa Ijumaa ya Juni 14 na babake ameeleza kinagaubaga kwa nini waliafikia kumpumzisha katika makaburi ya Lang'ata.

Muhtasari

• Njambi alifariki tarehe 3 Juni alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa endometriosis.

 

Njambi Koikai
Njambi Koikai
Image: Facebook

Sasa ni rasmi kwamba mkali wa muziki wa Reggae, Mary Njambi Koikai maarufu ka ma Fyah Mummah Jahmby atapumzishwa katika malazi yake ya milele makaburini Lang'ata mwishoni mwa juma hili.

Haya ni kwa mujibu wa babake ambaye alizungumza kwa kusononeka pakubwa na kufichua ratiba ya mipangilio ya mazishi ya binti yake aliyeaga baada ya kupambana na ugonjwa wa Endometriosis kwa miaka mingi.

Babake Njambi alifichua kwamba ibada ya wafu itafanyka Alhamisi na kufuatiwa na maziko katika makaburi ya Lang'ata siku itakayofuata ya Ijumaa, Juni 14.

Mzee huyo aliweza kujibu kinagaubaga kuhusu maswali ya wengi waliotaka kujua ni kwa nini waliafikia kumzika Njambi katika makaburi ya Lang'ata na si kijijini kwao kwa watu wa ukoo wa babake.

Akijibu swali hili, mzee huyo alisema kwamba familia ilionelea Njambi kuzikwa katika makaburi ya Lang'ata kwani marehemu bibi yake pia alizikwa huko na watamzika karibu na kaburi la bibi yake.

“Ibada ya ukumbusho itakuwa Alhamisi, na maelezo zaidi yatatolewa kabla ya mazishi Ijumaa katika Makaburi ya Lang’ata. Atazikwa huko kwa sababu bibi yake amezikwa huko, na familia ilitaka azikwe karibu naye," babake marehemu alieleza.

"Inasikitisha sana kumzika mtoto ambaye bado ni mdogo kwa sababu si baba anayepaswa kumzika mtoto; mtoto ndiye anapaswa kumzika baba," mzee baba aliongeza.

Njambi alifariki tarehe 3 Juni alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali moja jijini Nairobi baada ya kuugua kwa muda mrefu ugonjwa wa endometriosis.

Njambi alifariki siku mbili baada ya kuandika ujumbe wa kutia wasiwasi kwa mashabiki wake ambapo alikuwa anaomba msaada wa damu.

baada ya kifo chake, watu mbalimbali aliotangamana nao humu nchini na kutoka nje ambao wengi wao ni wapenzi wa muziki wa Reggae walimuomboleza kama mtu aliyekuwa mcheshi katika kazi yake ya upambe wa Reggae.

Dadake Njambi pia alimwandikia ujumbe mzito huku akitangaza kufariki kwa mwanahabari huyo.

Roho yake ipumzike kwa amani.