Aunty Ezekiel: Sina mpango wa ndoa na Kusah, akitaka kuoa aniambie!

"Ndoa hapana na hata yeye [Kusah] anajua kwangu mimi ndoa sitaki. Lakini yeye ni mvulana kama itafika siku atataka kuoa basi tutazungumza mimi na yeye, ila kwangu mimi imetosha,” Ezekiel alifafanua

Muhtasari

• Aunty Ezekiel akiwa kama moja kati ya mihimili mikuu katika safari ya mafanikio ya muziki wa Kusah, alisema kwamba kwa maoni yake wala asingependa msanii huyo kufika kilele.

Kusah na Aunty Ezekiel
Kusah na Aunty Ezekiel

Muigizaji wa muda mrefu wa filamu za Kiswahili maarufu kama ‘Bongo Movie’, Aunty Ezekiel katika mahojiano ya kipekee na runinga ya Global TV Online amefichua kwamba uhusiano wake na msanii Kusah hauna mustakabali wowote wa ndoa.

Katika mahojiano hayo, Aunty Ezekiel alisema kwamba uhusiano wake na msanii huyo wa kibao cha ‘I Wish’ ni wa kawaida tu wala yeye hana mpango wa kuja kuupaisha hadi kiwango cha ndoa, akisema kwamba Kusah yuko radhi kuoa mwanamke mwingine kama atataka ndoa, lakini kwake suala la ndoa hapana.

Ezekiel alisema kwamba sababu ya kutotaka kuishia katika ndoa na Kusah ni kutokana na kile ambacho kimekuwa kikionekana kama mtindo kwa wasanii wengi ambao huachana muda mchache baada ya kuoana, kwa hiyo ni bora tu yeye na Kusah waishi kama wachumba na wala si wanandoa.

“Niseme tu Mungu amenijaalia kumpata Kusah. Kusah japo kuwa ana umri mdogo yeye ni baba mzuri sana ambaye ana huruma, upendo... unavyomkuta ako na watoto unawaona watoto kabisa wana furaha sana japo kuwa hatujazaa naye. Ni baba mzuri sana, anajukumika kwa familia yake.”

“Mimi naamini kwamba umri si kitu, ila kuhusu ndoa kwa kweli hapana. Ameshakuwa baba bora tunakaa vizuri kwa nini ndoa? Tumeshaona watu wanaona siku mbili siku tatu wameachika, hauoni kama tunamchezea Mungu. Ndoa hapana na hata yeye [Kusah] anajua kwangu mimi ndoa sitaki.”

“Lakini yeye ni mvulana kama itafika siku atataka kuoa basi tutazungumza mimi na yeye. [Kuhusu kunioa mimi] hapana, mimi imetosha,” Ezekiel alifafanua.

Aunty Ezekiel akiwa kama moja kati ya mihimili mikuu katika safari ya mafanikio ya muziki wa Kusah, alisema kwamba kwa maoni yake wala asingependa msanii huyo kufika kilele cha kuwa nambari moja na pia hataki kumuona akiburuta mkia, bali angependa kumuona hapo katikati.

“Binafsi mimi nisingependa afike juu kabisa na kuwa namba moja, na pia nisingependa kumuona akiwa wa mwisho. Ni kama mimi tu nilishajikubali kuwa sitaki kuwa wa kwanza lakini pia mimi si namba sifuri. Kukaa namba moja kwa muda mrefu ni kazi, kuna namba moja wengi tumewaona wakishuka, sitamani awe namba moja, nataka awe katika nafasi nzuri, hiyo inatosha kabisa,” Ezekiel alisema.

Kusah na Aunty Ezekiel
Kusah na Aunty Ezekiel
Kusah na Aunty Ezekiel
Kusah na Aunty Ezekiel