Hatimaye Kevin Bahati aliweka wazi kuhusu hatua yake ya kuposti picha ya kumbukumbu ya mke wake Diana Marua na Victor Wanyama.
Baba huyo wa watoto watano alizua mzozo mnamo Juni 3, 2024 aliposhiriki picha hiyo na wakenya wengi bila kujua kuwa huo ulikuwa mpango wa kutangaza kipindi chao kipya cha Netflix, 'The Bahati's Empire'.
Wakati wa mahojiano na Betty Kyallo kwenye TV 47, wanandoa hao walizungumza kuhusu picha hiyo ya mtandaoni na Bahati alisema kuwa yeye na Wanyama walikuwa marafiki.
“Kwa nini nimuulize Wanyama ikiwa naweza kuweka picha ilhali ni yeye na rafiki yake? Ngoja nikuambie kitu. Sikuwahi sema chochote. Wanyama na Mariga ni marafiki zangu. Hata nilimfanyia kampeni Mariga huko Kibra."
"Wakati fulani unaona fununu, na unapokuwa kimya, zinachochea uvumi zaidi. Lakini unapoonyesha watu kwamba ni kawaida, watakaa kimya," alisema.
Alimalizia kwa kueleza kuwa alijiepusha kuzungumzia tuhuma hizo ovu ili kumlinda kila aliyehusika, hasa mtoto wake wa kulea.
"Wengi wa mashabiki wangu wanajua kuwa nilimuasili mwanangu. Picha ilipokuwa ikivuma kitambo, sidhani Wanyama alikuwa na ngozi nene kama mimi, na kwa hivyo siku moja ilikuwa ikivuma na ni ulimwengu katili wa mitandao ya kijamii.”
‘’Ilimpata. Ikiwa ningetoka kuishughulikia, haingesaidia mtu yeyote. Nilichagua kuwa kimya kuhusu hilo na kuendelea,” Bahati alieleza.
Kwa upande wake, Diana pia alifichua kukerwa kwake na mizozo ya mara kwa mara ya watumiaji wa mtandao kuhusu urafiki wake.
“Hutaki niwe na marafiki? Siwezi piga picha na watu, au ni kwa sababu yeye ni mtu mashuhuri?" Marua aliuliza.
Siku chache baada ya utangazaji wao, Diana alisema kwa ujasiri kwamba angekaa na Bahati kwa ajili ya wale wanaomchukia.
Kupitia chaneli yake ya YouTube mnamo Jumatano, Juni 5, Diana alisema, "Yaani ile siku nimekosana na Baha, yani nahisi amenifika hapa - akielekeza kwenye ncha ya ulimi - naskia ni kama naweza mtema" akicheka "hebu niambie nitamshika mtu wangu, nita...nitakaa na huyo mwanaume kwa ajili yenu nyie mnaotaka kuona anguko letu nawaambia bure."
Pia alifichua kuwa mchezo huo uliibuliwa na wafanyakazi wanaofanya kazi katika EMB Records ambayo mume wake anamiliki.