Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino alimtembelea mtetezi mkali wa sera za chama cha ODM na muungano wa upinzani wa Azimio, Nuru Okanga katika kituo cha polisi anakoshikiliwa kwa takribani wiki sasa.
Owino alitumia nafasi yake ya siku ya Eid-Al-Adha kutembelea wafungwa katika kituo cha Muthaiga jijini Nairobi ambapo Okanga anashikiliwa kwenye korokoro baada ya kutiwa mbaroni wiki jana kwa kile kinadaiwa na matamshi ya kudhalilisha dhidi ya viongozi wakuu serikalini.
Owino alipiga picha na Okanga alikuchukua mkate katika kituo hicho na kusema kwamba katika ziara yake kituoni Muthaiga, aliweza kulipa dhamana kwa wafungwa wengine 27 lakini akafichua kwamba polisi walidinda kumuachilia Okanga wakisema ni maagizo kutoka juu.
“Leo, Nilimtembelea Nuru Okanga katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga. Okanga alikamatwa kwa kuwaambia Ruto na Gachagua ukweli kuhusu Gharama ya Juu ya maisha na Mswada wa Kifedha.”
“Hakuweza kuruhusiwa kwa dhamana ya polisi kwa sababu maofisa hao wanadai kuwa Kesi imetoka Juu. Who else ako Juu Kama sio Mungu?Wonders will never end!!” Owino alifichua.
Wiki jana, Okanga alichapisha kwenye ukurasa wake wa Facebook akiwataarifu wafuasi wake kuhusu kukamatwa kwake, na kusema kwamba hakuwa anajua alikokuwa anapelekwa na kiini cha kukamatwa kwake na polisi.
“Nimekamatwa na Kupelekwa kusikojulikana. Sababu bado haijulikani,” alisema.