Nuru Okanga aomba msaada kwa matibabu ya mwanawe

"Hata kama ni shilingi moja itasaidia. Msipende kuchangia mtu wakati ako tuu na matanga.Niko na stress nyingi nitashukuru msaada wako," aliongeza.

Muhtasari

•Mwanaharakati wa kisiasa Nuru Okanga anatafuta usaidizi wa kulipa bili za hospitali na wauguzi wa mtoto wake.

•Mtoto wa Okanga aligunduliwa kuwa na tatizo la figo na amelazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta kwa wiki tatu sasa.

•Okanga, ambaye hivi majuzi alikamatwa na kuzuiliwa na polisi kwa zaidi ya wiki moja, aliwataka Wakenya kumsaidia kulipa bili za matibabu ya mwanawe.

ndani ya studio za Radio Jambo.
Nuru Okanga ndani ya studio za Radio Jambo.
Image: RADIO JAMBO

Mwanaharakati huyo wa masuala ya kisiasa amefichua kwamba mtoto wake wa kwanza wa kiume alipatikana na tatizo la figo na anaomba msaada kutoka kwa wakenya.

Mfuasi huyo wa Azimio la Umoja alikamatwa Juni 11 na kuzuiliwa chini ya ulinzi wa polisi kabla ya Babu Owino kumuokoa.

Okanga alifichua kwamba afya ya mtoto wake ilikuwa ikizorota wiki tatu baada ya kulazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta.

 “Mtoto wangu ako mbaya sana mwanzo walikuwa wameniomba ninunue chupa saba za dawa, lakini baadaye daktari akaniambia anahitaji nyingine tisa, akitumai angekuwa bora, lakini kwa bahati mbaya, chupa moja inagharimu KSh 10,000," alisema.

Okanga aliingia kwenye mtandao wake wa TikTok ili kuchangisha pesa za matibabu ya mwanawe.

Baba huyo wa watoto wawili aliwahimiza viongozi wa Azimio kumsaidia kulipa bili za hospitali ya mwanawe.

"Tafadhali niunge mkono. Nionyeshe uungwaji mkono jinsi ulivyonionyesha kila mara linapokuja suala la kutetea haki za Wakenya.

Nisaidie mwanangu angali hai. Usingoje afe ndio anitumie mamilioni," aliomba.

Okanga alisema alihofia huenda akampoteza mwanawe iwapo hatapata matibabu kwa wakati.

"Hata kama ni shilingi moja itasaidia. Msipende kuchangia mtu wakati ako tuu na matanga.

Niko na stress nyingi nitashukuru msaada wako," aliongeza.