Mwimbaji Tyla ashinda tuzo mbili za BET

Alichukua tuzo za Msanii Bora Mpya na Msanii Bora wa Kimataifa.

Muhtasari

•"Hii ni zawadi kubwa kuwepo hapa. Ningependa kutolea tuzo hii kwa Afrika." Alisema Tyla.

•Ushindi wake maradufu ulithibitisha nafasi yake kama nyota anayechipuka kwenye muziki wa Kiafrika na kimataifa.

Msanii Tyla akiwa amebeba tuzo ya BET
Image: HISANI

Mwanamuziki wa Afrika Kusini Tyla alitangazwa kuwa Msanii Bora Mpya kwenye Tuzo za BET 2024 siku ya Jumatatu.

Wimbo wake wa kwanza, 'Water', ulimfanya apate umaarufu wa kimataifa na kupata tuzo kadhaa, ikiwemo Tuzo ya Grammy ya Kwanza kabisa kwa Utendaji Bora wa Muziki wa Kiafrika mwezi Februari 2024.

Akiwa na umri wa miaka 22, alikuwa msanii mdogo zaidi barani Afrika kuwahi kupokea Grammy.

Akipokea tuzo ya Msanii Bora Mpya, ambalo alishinda dhidi ya washindani wake kutoka Afrika kama Ayra Starr, 4Batz, Bossman Dlow, Fridayy, October London, na Sexyy Red.

Katika hotuba yake ya kukubali tuzo, Tyla alisema, "Hii ni zawadi kubwa kuwepo hapa. Ningependa kutolea tuzo hii kwa Afrika.

Vilevile, ningependa kuitolea tuzo hii kwa nyota wote wa Kiafrika walionitangulia ambao hawakupata fursa kama ninazopata mimi. Hii ni ya kushangaza sana. Afrika kwa dunia marafiki zangu."

Pia alishinda tuzo ya Msanii Bora wa Kimataifa, akiwashinda nyota Asake, Ayra Starr, Aya Nakamura (Ufaransa), na wasanii wengine kutoka sehemu mbalimbali za dunia.

Ushindi wake maradufu ulithibitisha nafasi yake kama nyota anayechipuka kwenye muziki wa Kiafrika na kimataifa.

Mbali na hayo, Burna Boy, Tems, na Seyi Vibes walipata mapendekezo katika makundi ambayo bado hayajatolewa tuzo katika hafla hiyo, huku wakionyesha uwepo na kutambuliwa kwa vipaji vya Kiafrika kwenye tukio hilo lenye heshima kubwa.