Stevo Simple Boy aeleza kwa nini hakushiriki maandamano ya Gen Z licha ya kujiita mtetezi

“Mimi ningependa rais Ruto anialike tukutane tufanye mazungumzo, kwa sababu yeye ni rais wa taifa na mimi ni rais wa wanyonge, kwa hivyo tukikutana tutapata suluhisho ni kitu kipi tunaweza kuwapa Wakenya na ni kipi wangetaka rais kufanya.”

Muhtasari

• Stevo hata hivyo alisisitiza kwamba yeye si Gen Z bali anachokifanya ni kuwasaidia kufikisha sauti na malalamiko yao kwa uongozi wa taifa.

Stevo Simple Boy
Stevo Simple Boy
Image: Facebook

Msanii Stevo Simple Boy ambaye amejibandika jina lingine kama ‘Rais wa Wanyonge’ amefunguka kwa kutoa sababu zake za kutoshiriki katika maandamano ya vijana wa Gen Z wiki yaliyoanza wiki mbili zilizopita, licha ya kujitambua kama mtetezi wao.

Stevo alisema kwamba hakukosa kushiriki maandamano hayo ya kupinga mswanda wa fedha wa mwaka 2024 kwa njia ya makusudi bali ni tatizo ambalo liliwapata wakaazi wengi wanaotumia barabara kuu ya Thika kuingia jijini Nairobi.

Ikumbukwe awali tuliripoti kwamba msanii huyo alisema amehama Kibera na kwenda kuishi mtaani Kasarani.

Simple Boy alisema siku ya maandamano ambayo ilishuhudia makumi ya wasanii wenza wakijitokeza kujiunga na vijana, alikuwa na kila sababu ya kutoka lakini barabara ya Thika ilikuwa imefungwa na polisi ambao walinuia kuzuia watu Zaidi kufika katikati mwa jiji.

“Kwanza wacha niseme mimi kama rais wa wanyonge, wiki iliyopita tulifungiwa na polisi hapa Thika Road. Hicho kitendo kilileta matatizo na nikasema wacha nishuke kwa gari niambie Wakenya wenzangu mimi kama rais wa Wanyonge, nilifungiwa kwa barabara sikufika mjini,” Stevo alijitetea.

Msanii huyo aliwatetea waandamanaji wa Gen Z akisema kwamba hawakuwa na makosa yoyote kwani walikuwa wanadai haki yao kwa mujibu wa katiba ya Kenya.

Kuhusu video yake akitoa rai kwa rais Ruto kumpa usikivu, Stevo Simple Boy alisema;

“Mimi ningependa rais Ruto anialike tukutane tufanye mazungumzo, kwa sababu yeye ni rais wa taifa na mimi ni rais wa wanyonge, kwa hivyo tukikutana tutapata suluhisho ni kitu kipi tunaweza kuwapa Wakenya na ni kipi wangetaka rais kufanya.”

Stevo hata hivyo alisisitiza kwamba yeye si Gen Z bali anachokifanya ni kuwasaidia kufikisha sauti na malalamiko yao kwa uongozi wa taifa.