Mwanaharkati Eric Omondi ameanzisha mchango kupitia wakfu wake wa SISI KWA SISI kwa ajili ya kumzawadi jamaa aliyesaidia katika kuopoa miili kutoka timbo lililogeuzwa kuwa eneo la kutupa taka la Kware, mtaani Embakasi.
Omondi alichapisha video akikutana na jamaa huyo anayetambulika kama Kyalo Wambua, na kuwaomba mashabiki wa Sisi kwa Sisi kufanya kama kawaida yao na kutuma michango yao kama njia moja ya kumuonyesha Kyalo kwamba jamii inamthamini kwa kitendo chake cha kujitolea.
Kyalo alisema kwamba kazi hiyo amekuwa akiifanya kwa muda na ni kwa kujitolea kuwasaidia watu ambao wapendwa wao wanapatikana wameanguka katika timbo hilo.
Mwanamume huyo alifichua kwamba mpaka sasa tangu wikendi iliyopita, ameopoa miili 13 kutoka timbo hilo.
“Shujaa sio watu wako kwa ofisi...Hawa ndio mashujaa. This guy Kyalo Wambua alijitolea na akaopoa miili 13 kutoka timbo la Kware Mukuru Kwa Njenga. TEAM SISI KWA SISI hebu tubadili maisha ya huyu bwana kabisa,” Omondi aliandika kweney video hiyo.
Eric akiomba watu wenye moyo wa kutoa kusalimia M-Pesa ya huyo jamaa, alimtaja kama shujaa akisema kuwa vitu ameona pale kwenye yale magunia vinaweza kuja na trauma, hivyo anahitaji kupata muda mzuri wa kwenda likizoni kutuliza akili na mawazo.
Kyalo amekuwa mtu wa kuzungumziwa tangu Ijumaa shughuli ya uopoaji ilivyoanza kwani yeye ndiye mtu wa pekee aliyepata ujasiri wa kuingia katika timbo hilo lililojaa taka na kufungua gunia moja baada ya jingine kujaribu kutegua kitendawili cha miili iliyokuwa imetupwa kwenye gunia.