Msanii ambaye pia ni mjasiriamali na mmiliki wa lebo ya muziki ya Kaka Empire, King Kaka kwa mara nyingne tena ameonyesha uhodari wake katika michezo ya bahati nasibu.
King Kaka ambaye si mgeni katika suala la kucheza Kamari alionyesha jinsi alikwachua karibia shilingi milioni moja za Kenya baada ya kubashiri matokeo ya fainali ya mchuano wa Euro akitumia shilingi laki tatu tu.
Kupitia Instagram yake, King Kaka alichapisha picha ya jinsi aliweka dau la shilingi 322,500 kwenye mchezo huo baina ya Uhispania na Uingereza, akiipa Uhispania nafasi ya kushinda ili kumpa kima cha shilingi 848,175.
Kwa bahati nzuri, Uhispania ilimfanyiia haki kwa kuichabanga Uingereza mabao 2-1 kwenye fainali hiyo iliyochezwa usiku wa Jumapili nchini Ujerumani.
Kufuatia matokeo hayo, King Kaka alijikwachulia dau nono la laki 8 na nusu na kuwashukuru wachezaji wa Uhispania kwa kuokoa laki 3 zake, kwani mechi hiyo ilikuwa ngumu na ilihitaji bao la dakika za lala salama kupata mshindi.
Wakati uo huo pia alimpa pole mkewe, Nana Owiti ambaye alikuwa anaishabikia Uingereza.
“Asante Uhispania @lamineyamal Pole Sana @nanaowiti,” King Kaka alisema.
Hii si mara ya kwanza kwa msanii huyo kuonyesha ustadi wake katika michezo ya bahati nasibu.
Mwezi Mei mwaka huu, King Kaka alikwachua mkwanja mrefu wa hela baada ya kubashiri sahihi mchuano wa nusu fainali ya kipute cha ligi ya mabingwa barani Ulaya baina ya Real Madrid na Bayern Munich.
Akisherehekea ushindi wake kwenye Instagram, King Kaka , alionyesha picha ya iliyothibitisha ushindi wake wa KSh 1.2 milioni kutoka kwa hisa ya KSh 655,000 ambapo alikuwa ameipa Real Madrid nafasi ya kuibuka mshindi.