Wikendi iliyopita, mchekeshaji Mulamwah alitimiza ahadi yake kwa mashabiki wake kuwafichulia sura ya mwanawe, Oyando Jr.
Mulamwah na mpenzi wake Ruth K walitangaza mapema Ijumaa kuhusu tukio hilo ambalo walilipangia Jumamosi alasiri.
Wakati wa kutambulisha sura ya mwanao, walipeperusha tukio hilo mbashara kwenye mtandao wa YouTube na kumpa zawadi kadha, ikiwa ni miezi mitano baada ya kuzaliwa.
“my main man ❤️❤️ oyando jnr God literally said GOTHA TENA .. hey beb , tumeumba magic ... @atruthk thanks for the heir ❤️ , asante kwa kunipa family,” Mulamwah alimshukuru mpenziwe.
Hata hivyo, Mulamwah si wa kwanza tangu kuanza kwa mwaka huu kufanya bonge la tafrija kwa ajili ya kutambulisha sura ya mtoto kwenye mitandao ya kijamii.
Mwishoni mwa mwezi Januari, mwanasosholaiti Amber Ray na mpenziwe Kennedy Rapudo waliandaa tafrija la kukata na shoka kwa ajili ya kufichua sura ya binti yao, Africanah kwa mashabiki wao mtandaoni.
Katika nukuu ya pamoja, wapenzi hao hawakuweza kujizuia ila kumrukia binti yao mrembo kwa maneno matamu.
"Anapokua, ninashuhudia mabadiliko ya roho mchanga katika safari ya maisha. Yeye si binti yetu tu; ni rubani mwenza wetu katika safari hii, akitufundisha masomo ya kina ya upendo, uthabiti, na dhamana isiyoweza kuvunjika. Hiyo inatuunganisha pamoja,” Yalisomeka maelezo ambapo Rapudo alikuwa akimsifu Amber Ray kwa kumtunza bintiye.
Kando na Amber Ray na Rapudo, mwezi Machi pia familia ya Kabi na Milly Wajesus walifichua kwa mara ya kwanza sura ya mwanao kwenye jamii ya mitandaoni.
Wawili hao walichukua zaidi ya miaka miwili tangu kuzaliwa kwa binti wao kabla ya kutambulisha sura yake kwa mashabiki wao.
"Tumefurahi sana kwamba hatimaye unajiunga na familia yetu ya mtandaoni. Tunahisi kama familia ya WaJesu sasa imekamilika na tunajua utakuwa mtu wa ajabu," Milly alisema, maneno yake yakielekezwa kwa mtoto mdogo.
Na mwezi wa Juni, Bahati na mkewe Diana Marua pia walitambulisha sura ya binti yao wa mwisho, Malaika kwenye jamii ya mashabiki wao mitandaoni, wakati ambapo walikuwa wanazindua kipindi chao cha uhalisia kwenye jukwaa la Netflix.
Utambulisho huo ulifikisha kikomo ngoja ngoja ya mashabiki ambao wamekuwa wakiwatania kuwaonyesha sura ya mwanao tangu 2022 alipozaliwa.