Guardian Angel: Kuongea katika ndoa kumenisaidia kupunguza msongo wa mawazo

"Kama kuna kitu unapitia, ongea na mke, kama huwezi kuongea na mkeo, tafuta mtu unajua anaweza kuelewa, na kama huyo hawezi kuelewa, kuna njia moja ile yenye huwa hairuki, enda uambie Mungu,” aliongeza.

Muhtasari

• Alisema kwamba endap mtu utashindwa kufunguka kwa mkeo, basi tafuta yule mtu ambaye una ukaribu naye na kama hayupo, kimbilia kwa Mungu.

Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Esther Musila na mumewe Guardian Angel
Image: YouTube

Msanii wa injili Guardian Angel amefichua jinsi amekuwa akijisitiri dhidi ya msongo wa mawazo haswa katika ndoa yake.

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani, Angel alisema kwamba kitu ambacho kimemsaidia kutojikuta katika mkondo wa unyongovu na msongo wa mawazo ni kuzungumza na mpenzi wake Esther Musila, kila mara anapohisi kuwa anapitia changamoto Fulani.

“Kwangu mimi nahisi kwamba haswa katika ndoa yangu kitu kimenisaidia ni kuongea kila kitu. Hakuna kitu nahisi kinaniumiza chenye siwezi kuzungumzia, tuseme mke wangu amesema au amefanya kitu, ambacho hakitokei kila wakati, mimi huhakikisha kama kuna kitu hakiendi sawa na kinanikwaza kwa moyo wangu, lazima niiongee,” Angel alisema.

Msanii huyo alisisitiza kwamba mazungumzo ndio njia pekee ya kupunguza msongo wa mawazo kwa mtu yeyote, akiwashauri watu haswa wanaume kukumbatia njia ya mazungumzo kutatua kinachowakwaza.

Alisema kwamba endap mtu utashindwa kufunguka kwa mkeo, basi tafuta yule mtu ambaye una ukaribu naye na kama hayupo, kimbilia kwa Mungu.

“Mazungumzo ndicho kitu kimenisaidia sana, na yeye pia ikiwa kuna kitu anahisi hakiendi poa sisi huongea kuhusu kila kitu. Kama Mungu amekusaidia kupata mtu ambaye mnaweza ongea, wewe ongea kaka. Usifiche kitu chochote ndani ya moyo wako, kiwe kibaya au kizuri, inakuwa njia moja ya kukusaidia kujiondolea mzigo wa vitu vimejaa kwa moyo wako.”

“Kuongea ndio kila kitu, mazungumzo ndio njia pekee ya kuweza kutangamana na wenzetu. Kama kuna kitu unapitia, ongea na mke, kama huwezi kuongea na mkeo, tafuta mtu unajua anaweza kuelewa, na kama huyo hawezi kuelewa, kuna njia moja ile yenye huwa hairuki, enda uambie Mungu,” aliongeza.