Rodgers Oloo Magudha, almaarufu Nairobi Birdman, kijana ambaye amekuwa gumzo mitandaoni kwa kutembea na wanyama aina ya ndege walio hai kichwani na mabegani kila wakati amevunja kimya chake kuhusu madai kuwa huenda ni mshirikina.
Akizungumza na blogu ya SPM Buzz, Magudha alisema kwamba hali hiyo ya kupendwa na ndege si uchawi bali hi asili tu.
Kijana huyo alisema kwamba baadhi ya masaibu ambayo amekumbana nayo kutokana na kutembea na ndege wake ni pamoja na kutengwa huku wengi wakiamini kwamba si kawaida ndege kuvutiwa na mtu na kutua katika kichwa na mabega yake.
"Nimekabiliwa na ubaguzi na shutuma nyingi. Haya ni asili tu. Haina uhusiano wowote na uchawi. Nina shauku ya asili tu. Huo ndio msukumo wangu," alieleza.
Kujitolea kwa Magudha kwa maumbile kunabaki kuwa msukumo wake mkuu, na anaendelea kuhamasisha udadisi na kuvutiwa na wale wanaokutana naye mjini.
Tangu apate umaarufu, Magudha amezua hisia tofauti. Wengi wameshangazwa na uwezo wake wa kutembea huku kunguru wakiwa wamemkaribia sana.
Wengine wamekisia kuwa huenda anatumia uchawi kuwaweka ndege hao.
Awali, Magudha alipokea kipande cha ardhi katika maeneo ya Konza City.
Zawadi ya ardhi ilitolewa wakati wa hafla ya matembezi ya kuwaelimisha wanaume kuhusu afya ya akili iliyoandaliwa na mcheshi Oga Obinna.
Zawadi hii ya ukarimu ilitoka kwa kampuni ya mali isiyohamishika kwa kutambua uwepo wake wa kipekee na kusaidia ustawi wake.
Mbali na ardhi hiyo, Obinna alichangia mabati 10 kumsaidia Magudha kuanza kujenga nyumba yake.