Seneta maalum Karen Nyamu hakuweza kuficha furaha yake baada ya mwenzake katika bunge la seneti Edwin Sifuna kusifia muonekano wake mpya.
Nyamu ambaye aliinuka kuchangia hoja yake katika mjadala wa madeni ya kaunti, alikuwa na muonekano tofauti.
Seneta huyo alibadilisha muonekano wa nywele zake kwa kuja na wigi jipya kabisa ambalo Sifuna alilisifia kuwa ni la dhahabu.
Nyamu alipeleka klipu hiyo ya Sifuna kwenye instastory yake na kuonesha furaha kiranja wa walio wachache kwenye seneti kumsifia.
"Kama ambavyo dadangu seneta Karen Nyamu amesema, ni sharti nikiri kwamba nilikuwa nusra nisimtambue kutokana na taji lake jipya la dhahabu, sikumbuki mara ya mwisho nilimuona akiwa na muonekano huu, lakini iko sawa," Sifuna alisema.
Nyamu kwa upande wake, alisema kwa utani kwamba Sifuna ambaye ni seneta wa jimbo la Nairobi alikuwa anajaribu kutumia lugha changamano kupitisha kauli kwamba alikuwa na muonekano wa moto.
"Seneta wangu wa Nairobi anajaribu kutumia maneno mengi ninaonekana wa moto kwenye wigi langu, ah sasa 'iko sawa' ndio nini?" Nyamu alitania.