Polisi TZ wadai msanii Mandojo alipatwa amejificha katika kibanda cha mbwa kanisani na kuuawa

Mlinzi wa kanisa hilo majira ya 5am alisikia mbwa wakibweka na kuvizia akamuona mtu amejifungia kwenye moja ya banda la mbwa hao na kuita usaidizi wa waumini waliofika kwa ibada ya kwanza kumkabili mtu huyo.

Muhtasari

• Polisi walisema kwamba walifika na kumchukua Mandojo hospitalini ambapo alifariki baadae akipata matibabu.

• Kijana huyo mlinzi kwa sasa yuko mikononi mwa polisi akisaidia uchunguzi dhidi ya mauaji ya Mandojo.

MADONJO.
MADONJO.
Image: HISANI

Jeshi la polisi nchini Tanzania limetoa taarifa kuhusu kifo chenye utata cha msanii mkongwe wa Bongo Fleva, Joseph Francis Michael maarufu kama Mandojo.

Mandojo alitangazwa kufariki siku tatu zilizopita kaitka hali ya utata, ambapo taarifa za awali zilidai alishambuliwa na halaiki baada ya kudhaniwa kuwa mwizi jijini Dodoma.

Kwa mujibu wa jeshi la polisi, Mandojo aliuawa katika majengo ya kanisa moja jijini Dodoma majira ya saa kumi na moja asubuhi.

Polisi walieleza kwamba mlinzi wa kanisa hilo majira ya 5am alisikia mbwa wakibweka na kuvizia akamuona mtu amejifungia kwenye moja ya banda la mbwa hao na kuita usaidizi wa waumini waliofika kwa ibada ya kwanza kumkabili mtu huyo.

“Alifariki akiwa anaendelea kupata matibabu katika hospitali kuu ya mkoa wa Dodoma. Siku hiyo ya tarehe 11 mwezi wa 8, 2024, majira ya saa kumi na moja alfajiri, Joseph Francis Michael maarufu Mandojo alikutwa ndani ya uzio wa kanisa katoliki parokea ya mtakatifu Wote lililopo Nzuguni B huku akiwa amejificha kwenye banda la mbwa…”

“…akiwa kwenye banda hilo, mlinzi wa kanisa alisikia mbwa wanabweka kwa nje ya kibanda chao na alipofika aligundua kuna mtu amejifungia ndani ya moja ya banda hilo. Alifungia mbwa ndani ya kibanda kimoja na kuanza kupambana na mtu huyo. Aliinitisha usaidizi kwa waumini waliokuwa wamefika kwa ibada ya kwanza ambao walifanikiwa kumdhibiti,” taarifa ilisema.

Polisi walisema kwamba walifika na kumchukua Mandojo hospitalini ambapo alifariki baadae akipata matibabu.

Kijana huyo mlinzi kwa sasa yuko mikononi mwa polisi akisaidia uchunguzi dhidi ya mauaji ya Mandojo.