• “Kwa hili ningependa kutangaza kuondoka kwangu Radio Maisha na Standard Group kwa ujumla mara moja. ' alitangaza.
Mtangazaji mwenye tajriba ya muda mrefu Esther Mwende Macharia ametangaza kuondoka katika stesheni ya Radio Maisha iliyoko chini ya mwavuli wa Shirika la habari la Standard PLC.
Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, Mwende ambaye amekuwa akifanya shoo ya vijana kila siku ya wiki kuanzia adhuhuri hadi alasiri alitoa tangazo hilo akishukuru shirika hilo la habari kwa muda aliofanya nao kazi.
Mwende alikuwa mmoja wa watangazaji waanzilishi wa Radio Maisha miaka 14 iliyopita na ameondoka siku moja tu baada ya stesheni hiyo kusherehekea miaka 14 ya kuwepo nchini Kenya.
“Kwa hili ningependa kutangaza kuondoka kwangu Radio Maisha na Standard Group kwa ujumla mara moja. Ningependa kuwashukuru wasimamizi wa shirika la Standard kwa fursa ya kukuza taaluma yangu na vile vile chapa yangu kwa miaka 14 iliyopita,” alisema.
Kando na kushukuru uongozi wa Standard PLC, Mama huyo wa watoto wawili wa kiume pia aliwashukuru mashabiki wake ambao asilimia kubwa ni vijana kutokana na kipindi ambacho amekuwa akiongoza kuhusiana na masuala na miziki ya kizazi kipya inayowiana na vijana.
“Muhimu zaidi nitoe shukurani zangu kwa MASHABIKI wangu kote nchini na kwingineko kwa kumshikilia Malkia. Nyinyi ni bora na ninawathamini sana ❤️. Kwa kusema hivyo, siwezi kusubiri kushiriki nanyi nyumba yangu inayofuata ili niweze kuendelea KUFANYA NINACHOFANYA BORA. Nimefurahiya zaidi tayari. Nawatakia kila la heri wenzangu wa Radio Maisha,” alisema.