• Mama huyo wa mtoto mmoja alitaka wachungaji kumuombea ili kuishinda changamoto hiyo, kwani imemwia vigumu hata kupata mwenzi wa maisha kutokana na hofu.
Msanii mwenye utata Justina Syokau ametoa ombi la msaada wa maombi ya wachungaji na wainjilisti kwa kile anachokidai kuwa ni tatizo la kuwaogopa wanaume.
Kupitia video moja ndefu inayoenezwa kaitka mitandao ya kijamii, msanii huyo alizungumza kwa hisia akisimulia jinsi ambavyo amekuwa akipitia changamoto ya kuwaogopa wanaume kwa miaka 11 sasa tangu alipoachana na aliyekuwa mpenzi wake.
Mama huyo wa mtoto mmoja alitaka wachungaji kumuombea ili kuishinda changamoto hiyo, kwani imemwia vigumu hata kupata mwenzi wa maisha kutokana na hofu yake kwa kila mwanamume anayemuongelesha.
“Kuna suala limekuwa likinisumbua, yaani jambo tu ambalo limekuwa likinisumbua sana kama mtu na unakuta wakati mwingine sina nguvu ya kulisema. Nimeona ni vizuri niliseme tu ili mnisaidie kimawazo, mniombee wachungaji mkutane mniombee kwa sababu hili jambo limenisumbua kwa miaka 11,” Syokau alifunguka.
“Ni zaidi ya miaka 11 ambapo nimekuwa peke yangu na upweke, na ninaogopa wanaume. Ambacho watu hawajui ni kwamba ndio ninaongea sana lakini ukweli ni kwamba nyuma ya pazi ninaogopa wanaume sana tangu nilipoachwa na ex wangu. Ni kama ninaogopa kuvunjwa moyo tena hadi ninajikuta kwamba wakati mtu ananitongoza nashtuka na ninakataa kuendelea na mazungumzo,” aliongeza.
Mama huyo wa kijana wa miaka 11 alielezea jinsi alitendwa kimapenzi na mpenzi wake wa zamani, akisema kuwa aliachika mwaka 2013 na kujikuta kwenye mitaa ya Nairobi baada ya kile alisema wazazi wake nyumbani walikataa kumkaribisha pia wakidai hawako tayari kuishi na binti mwenye mtoto.