Esther Musila afichua kwa nini Guardian Angel hana mpango wa kusaini wasanii 7Heaven

Alisema kuwa 7 Heaven kwa sasa haiwezi kutajwa kama studio ya kibiashara ambayo mtu yeyote anaweza kuingia na kulipa kurekodi wimbo na kisha kutoka bali ni wao wanachagua ni nani wa kufanya kazi naye.

Muhtasari

• “Lakini kama unataka kufanya kazi na sisi, Guardian ana uwezo wa kukuongoza, lakini kama unahisi kwamba huhitaji muongozo wake ni sawa pia."

Esther Musila na Guardian Angel
Esther Musila na Guardian Angel
Image: Instagram

Esther Musila, mke na meneja wa Guardian Angel amefichua kwa nini lebo ya 7Heaven imesalia bila msani yeyote takribani mwaka mmoja baada ya kuzinduliwa.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya usiku wa tafrija ya injili katika mgahawa wa Sankara, Musila alifichua kwamba mwanzoni walikuwa na mpango wa kusaini wasanii kadhaa wa injili lakini ilifika mahali ikabidi wabadilishe mtazamo wao kuhusu hilo.

“7 Heaven ilizinduliwa Oktoba mwaka jana, bado hatujamaliza mwaka. Awali, lengo letu lilikuwa ni kusaini wasanii lakini tulifika mahali tukaamua kwamba hapana, hatutaki kumshikilia mtu, tunataka kumpa kila mtu uhuru wake kufanya chochote,” alisma.

“Lakini kama unataka kufanya kazi na sisi, Guardian ana uwezo wa kukuongoza, lakini kama unahisi kwamba huhitaji muongozo wake ni sawa pia. Ndio maana hatutaki kusaini wasanii, tunawapiga jeki tu kwa sababu Guardian ako katika biashara ya muziki, hivyo ndivyo anatoa sapoti yake,” Musila aliongeza.

Alisema kuwa 7 Heaven kwa sasa haiwezi kutajwa kama studio ya kibiashara ambayo mtu yeyote anaweza kuingia na kulipa kurekodi wimbo na kisha kutoka bali ni wao wanachagua ni nani wa kufanya kazi naye.

Guardian Angel alifanya tamasha lake la kwanza aliloliandaa na mkewe kwa jina Gospo 1 katika mgahawa wa Sankara usiku wa Jumamosi.