Mfanyibiashara na mwanasiasa Mike Sonko ameweka wazi nia yake ya kuanza safari ya kupunguza uzani wa mwili wake.
Kupitia kurasa zake katika mitandao ya kijamii, Sonko alichapisha video akitembea ndani ya gym yake na kusema kwamba anataka kuanza safari ya kupunguza uzito wa mwili wake.
Gavana huyo wa zamani wa Nairobi alisema anatafuta mkufunzi wa mazoezi ya gym wa jinsia ya kike, akisema kitambi chake kimekuwa kikubwa kupita kiasi na kuna haja yake kukipunguza kupitia mazoezi.
“Hii kitambi yangu sasa imekuwa too much. Natafuta mkufunzi wa kike wa mazoezi ya viungo kwa haraka. Mkufunzi wa mazoezi ya viungo vya kike akuje haraka upesi,” Aliandika kwenye video alizochapisha kwenye X akipapasa kitambi chake.
Katika chapisho lingine, Sonko alionekana akitembea kwa miguu na kufichua kwamba alilazimika kutembea zaidi ya kilomita tatu kama njia moja ya kupunguza uzai wake.
“Jana nilitembea 3laps za 3.7kms nikahema kama punda,” Sonko alifichua.
Hata hivyo, alisema kwamba baada ya kuweka wazi nia yake ya kuanza safari ya kupunguza uzani wa mwili, baadhi ya watu walimpa mapendekezo ya kutumia njia rahisi ya kumeza tembe za kukata uzani kuliko kuhangaika kufanya mazoezi kwenye gym.
Wengine walimshauri kufanyiwa utaratibu wa kufunga matumbo yake kama alivyofanyiwa mtangazaji Willis Raburu na balozi Big Ted.
“Sasa kuna baadhi ya marafiki wananiambia ati niende nikafanyiwe gastric bypass kama Bigted ama nifanyiwe upasuaji au nimeze puto kama Gavanaree, Raburu,” alifichua.