• “Lakini tuliishi pamoja, tuliomba pamoja, tuliamini pamoja na baadae tukaondokea maisha ya benchi,” aliongeza.
• Mchungaji huyo aliwaasa vijana kujitwika ujasiri wa kipekee na kutenga tarehe ya kufunga harusi.
Mensa Otabil, mchungaji maarufu kutoka taifa la Ghana amezua mjadala pevu katika mitandao ya kijamii baada ya video kutoka mojawapo ya mahubiri na mafundisho yake kwa vijana kuenezwa mitandaoni.
Mchungaji huyo wa kanisa la Innternational Centre Gospel Church, ICGC katika mafundisho yake, aliwashauri vijana kwa kuwataka kufikiria kufunga harusi na kutulia kwenye ndoa hata kama hawana chochote kwa jina lao.
Mchungaji Otabil aliwataja vijana wanaosubiri kupata utajiri ili kuoa kuwa vichwa vyao vina kasoro kubwa, akisema kuwa utajiri unafaa kuja baadae ukiwa kwenye ndoa.
“Kama unasubiri kupata utajiri ili uoe kichwa chako hakifanyi kazi. Hamtaki kuoana lakini mnalala pamoja. Ambacho kimehifadhiwa kwa ajili ya ndoa unakitaka lakini hutaki kupitia mchakato halali wa kukipata. Kichwa chako kina kasoro,” Mchungaji huyo alifoka.
Mzee huyo wa umri wa miaka 64 alitoa mfano kwamba wakati wa ujana wake alipoamua kufunga ndoa, hakuwa anamiliki chochote zaidi ya mavazi machache tu.
“Wakati nilikuwa nafunga ndoa, mke wangu anaweza kuwaambia, sikuwa na chochote. Sikuwa na kitanda, viti wala vyombo vya jikoni. Fenicha ya kwanza katika chumba chetu ilikuwa ni benchi ambazo zilikuwa zimetupwa kutoka kanisani,” alisimulia.
“Lakini tuliishi pamoja, tuliomba pamoja, tuliamini pamoja na baadae tukaondokea maisha ya benchi,” aliongeza.
Mchungaji huyo aliwaasa vijana kujitwika ujasiri wa kipekee na kutenga tarehe ya kufunga harusi.
“Kuwa na ujasiri wa kuoa. Tenga tarehe na kama mnaogopa kuhusu kupata shela, keki, chakula, msikuwe na shaka. Fanya kuja katika ofisi ya kanisani na tunamaliza taratibu zote, basi. Kutoka hapo kila kitu kitakuwa sawa,” alisema.
“Baada ya kufunga harusi na kuishi katika ndoa takatifu, utaanza kuona kwamba vita ambavyo unapigana kimaisha kwa sasa vitakuwa rahisi kwako kushinda. Hivyo ndivyo wazazi wenu walifikia walipo sasa hivi,” aliongeza.