“Kando na kuingia TikTok kusema ‘tap tap’ bado natangaza neno la Mungu” - Ringtone

"Hivyo nilienda pale ili wakati watu wanaongelelea maneno chafu ya kidunia, niwe yule mtu mmoja wa Yesu wa kusema ‘tap the screen Yesu atakubariki, anakupenda, Yesu anakuja’, unaona?” Ringtone alifafanua.

Muhtasari

• Msanii huyo pia alisema kwamba haoni kama kuna lolote baya analifanya kuingia katika mtandao huo na kuomba kupatiwa zawadi.

 

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Msanii wa injili mwenye utata, Alex Ringtone Apoko amejitokeza na kutetea uamuzi wake wa kujiunga na mtandao wa video fupi wa TikTok, miezi kadhaa baada ya kukejeli mtandao huo.

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani, Apoko alikiri kwamba ni kweli ameingia TikTok lakini akaitaja kama fursa adimu ya kuwafikia watu nyakati za usiku kwa neno la Mungu wakati ambapo wengi wao wanafanya vitendo alivyovitaja kama ‘visivyofurahisha machoni pa Mungu’.

“Niko pale TikTok kwa sababu nilipata fursa ya kupata watu usiku mahali watu wanasema maneno ya nguoni. Hivyo nilienda pale ili wakati watu wanaongelelea maneno chafu ya kidunia, niwe yule mtu mmoja wa Yesu wa kusema ‘tap the screen Yesu atakubariki, anakupenda, Yesu anakuja’, unaona?” Ringtone alifafanua.

Msanii huyo pia alisema kwamba haoni kama kuna lolote baya analifanya kuingia katika mtandao huo na kuomba kupatiwa zawadi.

Alisema kuwa imekuwa kama sheria kwa yeyote anayeingia LIVE TikTok kuwa ni lazima aitishe zawadi, na akafichua kuwa ukweli huwa anazawadiwa lakini zaidi ya kila kitu, lengo kuu ni kumhubiri Mungu kwa wanaTikTok.

“Hivyo mimi nilipata fursa ya kumhubiri Mungu lakini pia pale TikTok sheria ni lazima uitishe zawadi za maua na simba. Sasa siwezi enda pale kuvunja sheria, napewa simba, maua lakini zaidi ya hayo ninatangaza neno la Mungu,” alijitetea.