•Gilda alimpongeza Guardian Angel na kueleza jinsi anavyojivunia mwimbaji huyo wa nyimbo za injili kutokana na tukio hilo lenye mafanikio.
•Alisema ilikuwa jambo nzuri kutangamana na mashabiki wa Guardian Angel na akawashukuru kwa sapoti yao.
Gilda Naibei, bintiye Esther Musila amemwagia sifa kemkem babake wa kambo Guardian Angel kufuatia tamasha lake ya hivi majuzi lililofanikiwa, Gospo1.
Katika mahojiano baada ya tamasha hilo la injili, mwanahabari huyo mwenye umri wa miaka 30 alimpongeza Guardian Angel na kueleza jinsi anavyojivunia mwimbaji huyo wa nyimbo za injili kutokana na tukio hilo lenye mafanikio.
Alisema mume huyo wa mamake aliafikia matarajio ya mashabiki na kufanya kila mtu kufurahia tamasha hilo.
“Mwanaume huyu! Aliiua (x3), nilitamani shoo hii haiwezi kuisha sasa hivi! Kama ingendelea… Lakini, ninajivunia wewe. Ulifanya kile ambacho kila mtu alitaka kusikia,” Gilda alisema.
Mrembo huyo alibainisha kuwa mwimbaji huyo wa nyimbo za injili alifanya mambo mengi na kupita kawaida ili kufanikisha shoo hiyo.
"Ninajivunia yeye sana, alifanya kila kitu; alikuwa DJ, alikuwa anaimba.. Namaanisha, hii ilikuwa shoo ya kiroho, na aliweza kuwapa watu kile walitaka. Watu walikuwa wakimsifu Mungu,” alisema.
Pia alisema kuwa ilikuwa jambo nzuri kutangamana na mashabiki wa Guardian Angel na akawashukuru kwa sapoti yao.
"Ikiwa unamsapoti Guardian, tuko naye 100%. Sisi ndio ambao huwa naye kawaida na huwa tunamwambia kila siku "unaweza kufanya hivi", lakini bila nyinyi mashabiki, nyinyi ni kila kitu," alisema.
Gilda alimaliza mahojiano hayo kwa kumtambua babake wa kambo kama supastaa.
Mrembo huyo ni mmoja wa watoto watatu wa Bi Esther Musila kutoka ndoa yake ya awali. Ana wengine wawili wanaojulikana kama Glen na Kim.
Katika mahojiano ya mapema mwaka huu na blogu ya hapa nchini, Guardian Angel alisema kwamba anahusiana vyema sana na watoto wote wa mke wake Esther Musila.
“Wao ni watu wakubwa. Tuko na uhusiano mzuri, uhusiano mzuri sana,” Guardian Angel alisema.
Kwa upande wake, Bi Esther Musila alifichua kwamba watoto wake waliingiana vyema sana na mumewe huyo wa miaka 35 tangu mwanzo
Aidha, alifichua kuwa .alipoanza kuchumbiana na mwimbaji huyo wa nyimbo za injili, watoto wake walibaini kwa urahisi kwani kulikuwa na mabadiliko makubwa katika tabia zake.
“Siku moja niliwaambia nachumbiana na mtu huyu. Unajua watoto tu, mimi nikiwa mzazi wao pekee, kulikuwa na dhana kwamba mama amepata mtu, tutaachwaje peke yetu? Lakini Guardian alikuja maishani mwao kwa kishindo. Tangu siku ya kwanza nilipomtambulisha kwao, walikuwa na maelewano mazuri,” alisema.