• Alisema kwamba atafanya hivyo kwa kuhama pia nchini Tanzania na kupeleka makao yake nchini Afrika Kusini katika taifa mama la chimbuko la Amapiano.
Msanii wa lebo ya Konde Music Worldwide, Ibrahim Abdallah Nampunga, maarufu kama Ibraah ametishia kubadilisha muziki pamoja na uraia kwa ujumla iwapo hatoshinda tuzo ya msanii bora wa mwaka huu nchini Tanzania.
Kupitia Instagram, msanii huyo wa pekee aliyesalia chini ya lebo ya Harmonize alisema kwamba anahisi amekubalika sana mtaani na mashabiki na hilo ni thibitisho tosha la kumshindia tuzo ya msanii bora wa mwaka.
Ibraah alisema iwapo mwaka huu hatoshinda tuzo hiyo katika hafla ya kutolewa kwa tuzo za Bongo Fleva, basi ataacha kuimba miziki ya Bongo Fleva na kuanza kuimba Amapiano.
Alisema kwamba atafanya hivyo kwa kuhama pia nchini Tanzania na kupeleka makao yake nchini Afrika Kusini katika taifa mama la chimbuko la Amapiano.
“Heshima ninayo ipata mtaani inatosha kuwa msanii bora kwa mashabiki zangu maana nafanya muziki kwaajili yao jua lizame lichomoze naitwa chingaa mwenye macho haambiwi ona. Bongo fleva ikininyima tuzo mwaka huu bora niimbe piano niwe msanii wa South Africa,” Ibraah alitishia.
Suala la jinsi tuzo za Tanzania Music Awards zinatolewa limekuwa likizua gumzo katika miaka ya hivi karibuni, baadhi ya wasanii wakilalamikia kila wanahisi ni kuwepo kwa upendeleo kwa wasanii katika vipengele Fulani.
Itakumbukwa wasanbii Rayvanny na Rosa Ree ni baadhi ya majina makubwa ambao walilalama vikali.
Rayvanny kwa upande wake alisonga mbele na kuwataka waaandaji wa tuzo hizo kumtoa kabisa katika vipengele vyote kwani hataki tena kushirikishwa, kauli sawa na Diamond aliyelalama miaka ya nyuma.