• Alialikwa kushiriki Miss Universe Nigeria baada ya nafasi yake kama mshindi wa fainali katika shindano la Miss Afrika Kusini kuzua wimbi la ukosoaji.
Baada ya kuandamwa juu ya uraia wake na kulazimishwa kujiondoa kwenye shindano la Miss Afrika Kusini, Chidimma Adetshina ametawazwa kuwa malkia wa urembo wa nchi tofauti kabisa.
Bi Adetshina alilia machozi ya furaha alipotangazwa kuwa Miss Universe Nigeria siku ya Jumamosi.
"Taji hili si la urembo tu; ni wito wa umoja," mwanafunzi huyo wa sheria mwenye umri wa miaka 23 alisema baada ya wiki kadhaa katikati ya dhoruba kali ya vyombo vya habari.
Alialikwa kushiriki Miss Universe Nigeria baada ya nafasi yake kama mshindi wa fainali katika shindano la Miss Afrika Kusini kuzua wimbi la ukosoaji.
Baadhi ya watu nchini Afrika Kusini walikuwa wametilia shaka kustahili kwake kushiriki katika mashindano ya urembo kwa sababu licha ya kuwa raia wa Afrika Kusini, babake Bi Adetshina ni Mnigeria na mamake ana asili ya Msumbiji.
Katika mahojiano Bi Adetshina alisema alizaliwa Soweto - kitongoji cha Afrika Kusini karibu na Johannesburg - na alikulia Cape Town.
Mzozo kuhusu uraia wake ulizua uchunguzi huku waandaji wa Miss Afrika Kusini wakiitaka idara ya mambo ya ndani ya taifa hilo kuangalia kustahiki kwake.
Baada ya uchunguzi wa awali, idara ilitangaza kuwa mamake Bibi Adetshina huenda alifanya "wizi wa utambulisho" ili kuwa raia wa Afrika Kusini.
Hata hivyo, taarifa hiyo iliongeza kuwa Bi Adetshina "hangeweza kushiriki katika madai ya vitendo vya kinyume cha sheria vya mamake kwani alikuwa mtoto mchanga wakati huo".
Siku moja baada ya tangazo hilo, Bi Adetshina alijiondoa katika shindano hilo, akisema alichukua uamuzi huo kwa ajili ya usalama na ustawi wa familia yake.
Kufikia sasa, masaibu yake yalikuwa yamegonga vichwa vya habari kote ulimwenguni.
Baada ya kusikia hadithi ya Bi Adetshina, waandaaji wa Miss Universe Nigeria walimwalika kushiriki katika shindano lao.
Walisema ataweza "kuwakilisha ardhi ya asili ya baba yake kwenye jukwaa la kimataifa".
Baada ya kushinda shindano hilo siku ya Jumamosi, Bi Adetshina atawakilisha Nigeria katika shindano la Miss Universe la Novemba.
Mafanikio yake yamesherehekewa kwenye mitandao ya kijamii.