Huku mfarakano kati ya mchungaji Ben Kiengei na mkuza maudhui Pritty Vishy ukizidi kupata nyufa zaidi, mchungaji wa kanisa la Salvation Healing Ministry, Victor Kanyari ameingilia kati.
Kanyari katika kipindi cha moja kwa moja kwenye TikTok, alijitolea kumsaidia Kiengei kwa ushauri.
Mchungaji huyo mwenye utata vile vile alimsuta Kiengei kwa kukejeli maumbile ya Pritty Vishy na kumshauri kwamba msamaha hauombwi mikono mitupu.
Kanyari alimtaka Kiengei kuzama zaidi katika akaunti yake ya kutoa laki 5 ili naye amcangie laki zingine 5 iwe milioni moja na wamkabidhi Pritty Vishy kama njia moja ya kumuomba msamaha wa kweli.
“Naona tumtafutie Pritty Vishy shilingi milioni moja, wewe utafute laki 5 na mimi 5 tumpe, huwezi enda kuomba msamaa mikono mitupu. Umesamtukana eti hana mwili mzuri,” Kanyari alishauri.
Haya yanakuja saa chache baada ya Kiengei kuomba msamaha kwa njia ya maandishi kwa Pritty Vishy akionekana kujutia matamshi yake wakati wa mahojiano kwenye video moja iliyozua ghadhabu mitandaoni.
“Pritty Vishy samahani sana na nachukua muda huu kukuomba radhi sana kwa kutaja jina lako kwenye onyesho ambalo nilipita juu na kukutaja kwa njia isiyo sahihi. Pata nafasi moyoni mwako kunisamehe kwa kukuhutubia kwa njia isiyofaa,” aliomba msamaha.
Ni msamaha ambao Vishy alionekana kuukataa, akisema kwamba hilo ni jambo alilolifanya kwa makusudi kabisa na hata kutishia kufika katika kanisa lake wikendi ijayo ili wakutane ana kwa ana.
“Ulipofungua sana mdomo wako kunitusi ulimtuma msaidizi wako ama ni yeye alikuandikia mstari? Ikiwa unataka kuzungumza nami zungumza nami moja kwa moja, na kabla ya hapo sitaki msamaha wa maandishi. Ninataka video, jinsi ulivyokaa chini na kutengeneza video hiyo isiyo na heshima, fanya vivyo hivyo wakati wa kuomba msamaha…usitume watu kwangu kwani walikusaidia kunicheka?” Alisema.