Kila mtu mwenye ako TikTok ni ombaomba - The Smart Joker

"Lazima uombe zawadi, na kama unategemea TikTok kwa mlo wako wa kila siku, huwezi kula kama hutageuka ombaomba,” Smart Joker alisema.

Muhtasari

• “Wakati wa Corona, hapo ndio maisha yalirudi chini na sasa watu wakaingia TikTok wanakaa kama omba omba.," Smart Joker alisema.

SMART JOKER.
SMART JOKER.
Image: FACEBOOK

Mchekeshaji Smart Joker ametoa maoni yake kuhusu watu wanaotumia mtandao wa video fupi wa TikTok kufanya vipindi vya moja kwa moja.

Akizungumza na mwanablogu wa Plug TV Kenya, Smart Joker alisema kwamba watu wote wanaotumia TkTok Live walianza tabia hiyo wakati wa janga la Covid-19 na kwamba wote sasa wamekuwa omba omba.

“Wakati wa Corona, hapo ndio maisha yalirudi chini na sasa watu wakaingia TikTok wanakaa kama omba omba. Kila mtu mwenye ako tiktok anaomba watu, siku yeyote mtu akienda Live, lazima ataomba watu. Kila mtu mwenye ako tiktok ni ombaomba. Namba moja, ili TikTok yako ifikie watu wengi, sharti uwabembeleze watu kupenda kipindi chako, pili lazima uombe zawadi, na kama unategemea TikTok kwa mlo wako wa kila siku, huwezi kula kama hutageuka ombaomba,” Smart Joker alisema.

Hii si mara ya kwanza kwa hulka ya omba omba kwenye TikTok imezua gumzo humu nchini.

Miezi kadhaa iliyopita, YouTuber Vincent Mboya pia aliibua kauli hiyo akisema tiktokers wengi wamegeuza mtandao huo kama jukwaa la kuomba omba zawadi za pesa na maua kutoka kwa mashabiki.

“Maceleb wa Kenya sasa imetosha, achene kuwatumia vibaya Wakenya na roho yao nzuri ya kutoa. Kama usanii umekataa, nendeni mfanye kazi, acha kuwa omba omba mchango. Na kama hauna kazi rudi kijijini. Kuingia tiktok live na kuomba gifts hiyo sio kazi,” Mboya alisema.

Mwanablogu huyo alitoa mfano jinsi mtandao huo ulikuwa wa burudani nzuri nyakati za mwanzoni na watu wa awali kama kina Azziad Nasenya, akisema kuwa hao ndio walikuwa wapakuaji wa burudani bila kuwalipisha mashabiki wao.

“TikTok ilikuwa ni furaha tupu kabla ya siku za kina Azziad, lakini siku hizi kila mtu tiktok ni ombaomba, tafakari wajinga sisi ambao tunatuma hizo zawadi, hebu na tugutuke kutoka usingizi na tuwalazimishe tiktokers hawa watuburudishe na sio kuwa ombaomba,” Mboya alisema.