“Mkijaribu kunyakua shamba la kanisa nitawaua na kesi nitajibu mbinguni” – Pasta Ng’ang’a

Ng’ang’a alisema atawatumia laana ya ugonjwa wa ukoma kama Naaman kwenye Biblia na watakufa wengi, akisema atajiandaa kujibu kesi yao mbinguni kwa Mungu.

Muhtasari

• " Hiki wakichukua, nitawaua watu wengi sana, watachomeka na ndege, watashikwa na kansa, nitawatupia ugonjwa wa Naaman."

Mchungaji Ng'ang'a atoa neno kwa wanaokosoa matamshi yake.
Mchungaji Ng'ang'a atoa neno kwa wanaokosoa matamshi yake.
Image: Screengrab//Sasa TV

Kwa mara nyingine mchungaji wa kaqnisa la Neno Evangelism, James Maina Ng’ang’a kwa mara nyingine ametema cheche za moto kwa baadhi ya watu ambao wanamezea mate ardhi linakokaa kanisa lake.

Katika video ya ibada ambayo inasambazwa mitandaoni, pasta Ng’ang’a aliwatishia wanyakuzi wa ardhi dhidi ya kufikiria kunyakua ardhi hiyo akisema kwamba wakijaribu kuiba shamba la kanisa atawatumia ugonjwa wa kifo.

Ng’ang’a alisema atawatumia laana ya ugonjwa wa ukoma kama Naaman kwenye Biblia na watakufa wengi, akisema atajiandaa kujibu kesi yao mbinguni kwa Mungu.

“Na hakuna siku mbwa itapokonya simba nyama, hiki kiwanja hakuna vile mtu anaweza kuchukua. Hiki wakichukua, nitawaua watu wengi sana, watachomeka na ndege, watashikwa na kansa, nitawatupia ugonjwa wa Naaman. Ukoma wa Naaman itawamaliza mpaka wajukuu wao. Kesi zingine nitajibu mbinguni,” Ng’ang’a alisema.

Mchungaji huyo mwenye misimamo mikali kuhusu ardhi ya kanisa lake alisema kwamba kwa muda amekuwa akipokea vitisho kutoka kwa watu walioko ndani ya serikali ambao wanatishia kuchukua shamba hilo.

Mapema mwaka hu, Ng’ang’a alitoa kauli kali dhidi ya serikali baada ya kudai kupokea barua ikisema kwamba ardhi linalokaa kanisa lake ni ya shirika la reli nchini na alitakiwa kuondoka.

Hata hivyo, kupitia kwa wakili wake, Silvanus Osoro, Ng’ang’a alisema alinunua shamba hilo zaidi ya miaka 20 iliyopita kutoka kwa benki kuu ya Kenya na kusema serikali yenyewe ndio ilitangaza ardhi hiyo kwenye gazeti rasmi la serikali.