• Msanii huyo alisema kwa kubadilisha mavazi, nywele na misamiati mipya, analenga kuwa kama Diamond, lakini si wa Afrika Mashariki pekee bali Diamond wa Afrika nzima.
Msanii Stevo Simple Boy kwa mara nyingine ametetea muonekano0 wake mpya wa kubadilisha mavazi na mtindo wa nywele.
Akizungumza na blogu ya Obinna TV, Simple Boy alisema kwamba ana damira kuu na kuna kitu anakilenga katika ubunifu wake mpya wa mavazi, mtindo wa nywele na hata misamiati ya kipekee.
Msanii huyo alisema kwa kubadilisha mavazi, nywele na misamiati mipya, analenga kuwa kama Diamond, lakini si wa Afrika Mashariki pekee bali Diamond wa Afrika nzima.
“Kama msanii, lazima mionekano yako ikuwe tofauti. Unajua watu labda wanauliza kwa nini Stevo Simplew Boy ameamua kubadilisha mavazi, nywele na hata kuja na misamiati mipya. Ni kwa sababu pia mimi nataka nikuwe international. Mimi ndiye Diamond wa Afrika. Diamond ni Simba wa Tanzania, lakini mimi ni Simba wa Afrika,” Stevo Simple Boy alifafanua.
Hivi majuzi, msanii huyo alifichua kwamba anatarajia kusafiri kwa ajili ya ziara ya kutumbuiza nchini Saudi Arabia kwa mara ya kwanza katika maisha yake.
Alisema kwamba alijishindia ziara hiyo shukrani kwa msamiati wake mpya – Mefi mefi muskla, akisema kwamba ni maneno ya Kiarabu yanayomaanisha ‘hakuna matata’.
“Kwa hiyo mefi mefi muskla ni lugha ya Kiarabu, wakati nilisema hivyo, unajua nini kilifanyika? Ni bahati tu ilinitokea, mwezi ujao ninaenda Saudi Arabia kwa kusema tu ‘mefi mefi muskla’. Tarehe 23 Septemba nitakuwa napiga shoo Riyadh. Mefi mefi muskla inamaanisha hakuna shida, mambo yaki shwari,” Stevo alifafanua zaidi.