Mimi nikipiga dili niingize Sh300m, nusu ni ya kusaidia watu – Mike Sonko

"Naeza pata hata Sh5m leo halafu nione kisa halali mtandaoni pengine mtu anaugua saratani, umaskini au mtu anaumia watoto hawana karo. Nitatumia hizo pesa zote kusaidia wananchi nibaki na sifuri,” Sonko aliongeza.

Muhtasari

• Sonko kwa muda mrefu amekuwa akijulikana kama mtu mwenye roho safi na moyo wa kuguswa na matatizo ya watu wa kawaida.

• Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijami, Sonko amekuwa akionyesha jinsi amekuwa akiwasaidia watu wenye matatizo ainati, kisa kilichogusa wengi kikiwa kile cha mtoto Satrine Osinya.

MIKE SONKO
MIKE SONKO
Image: Screengrab

Mfanyibiashara na mwanasiasa Mike Sonko amefichua kwamba yeye katika kila pesa anazotengeneza, nusu huwa zinakwenda katika kusaidia watu na nusu nyingine husalia katika kuendesha biashara zake na familia.

Akizungumza na waandishi wa habari za burudani wikendi iliyopita katika tamasha ya jamii ya Akamba, Sonko alisema kwamba hiyo imekuwa tabia yake katika kila pesa anazoingiza kutoka kwa dili zake zote.

“Huku kusaidia kwetu huwa ni kwa muda, kuna wakati Mungu anaweza nibariki nipige dili ama niuze kashamba nipata kama 200m au 300m. nusu ya hizo pesa nitapeleka kwa familia na kufanya mambo yangu, starehe zangu na sherehe zangu na nusu nyingine sharti iende kwa kusaidia watu,” Sonko alisema.

“Huyo ni Sonko. Naeza pata hata Sh5m leo halafu nione kisa halali mtandaoni pengine mtu anaugua saratani, umaskini au mtu anaumia watoto hawana karo. Nitatumia hizo pesa zote kusaidia wananchi nibaki na sifuri,” Sonko aliongeza.

Sonko alisema kuwa kwa filosofia yake, pesa ni karatasi tu na hakuna hata mmoja amewahi fariki akazikwa pesa, akitolea mifano baadhi ya watu matajiri waliotangulia mbele za haki.

“Nikishasaidia hivyo, Mungu hunibariki na zingine. Mimi huwa sithamini pesa kwa sababu hizo ni karatasi tu. Mtu hawezi zikwa na pesa zake,” Sonko alisema.

Sonko kwa muda mrefu amekuwa akijulikana kama mtu mwenye roho safi na moyo wa kuguswa na matatizo ya watu wa kawaida.

Kupitia kurasa zake za mitandao ya kijami, Sonko amekuwa akionyesha jinsi amekuwa akiwasaidia watu wenye matatizo ainati, kisa kilichogusa wengi kikiwa kile cha mtoto Satrine Osinya.

Kwa wale wasiojua, Satrine ni mtoto ambaye Sonko aliamua kumuasili baada ya mamake kupigwa risasi na kufa akiwa kanisani naye, kipindi hicho mtoto huyo alikuwa na mwaka mmoja na nusu na alikuwa ubavuni mwa mamake wakati majambazi wanaokisiwa kuwa wanamgambo wa Al Shabaab walipovamia kanisa la Joyland huko Likoni na kuuwa makumi ya waumini.