Bahati aeleza sababu ya kuachilia wasichana wawili alio’adopt pamoja na Morgan

“Ilikuwa ngumu kwangu kwa sababu hawakuwa na familia, mama yao hakuwa vizuri, hivyo nilifanya uamuzi mgumu wa kubaki na Morgan na kuwarudisha wasichana wawili kwa kituo cha watoto mayatima,” Aliongeza.

Muhtasari

• Hata hivyo, Bahati alifichua kwamba miaka kadhaa baadae, alifurahia kukutana na wasichana hao katika muunganik uliojaa hisia tele.

• "Na leo Purity na Rose wametutembelea na najua wamekuwa wakipitia maisha magumu sana,” Bahati alisema huku akienda kuwakaribisha mabinti hao nyumbani kwake.

 

MORGAN NA BAHATI
MORGAN NA BAHATI
Image: HISANI

Msanii Bahati Kioko kwa mara ya kwanza amefichua sababu iliyomfanya kuachilia wasichana aliowachukua pamoja na Morgan kuwalea, takribani miaka 10 iliyopita.

Akizungumza kwenye video katika chaneli ya mpenzi wake, Diana Marua, Bahati alifichua kwamba huenda wengi wasijue lakini wakati alijipata kimaisha, aliamua kurudisha mkono kwa jamii kwa kuchukua watoto 3 wasio na wazazi –wasichana 2 na mvulana 1- kuwalea.

Hata hivyo, baadae ilimkalia vigumu kuendelea kuishi na mabinti katika nyumba moja na kufanya uamuzi mgumu wa kuwaachilia na kusalia na mvulana – Morgan Bahati.

“Wakati nilimchukua Morgan kama mwanangu, nilimchukua pamoja na wasichana wawili; Rose na Purity. Walikuwa watoto wadogo sana na wakati huo kusema kweli nilikuwa mdogo sana kiumri. Ndio nilikuwa nimeanza muziki pia nilikuwa bado najitafuta hapa na pale kutafuta riziki. Kisheria sikuwa bado nimefikia umri wa kuweza kuruhusiwa kuasili watoto na haswa watoto wasichana,” Bahati alisimulia.

“Lakini ilifikia wakati ilinibidi kufanya moja kati ya maamuzi magumu kabisa maishani mwangu, hili liliniuma sana. Nilihisi kwamba niko katika hali ngumu kwa sababu sikuwa nimelindwa kisheria kuishi na watoto wa kike. Hata kama nilikuwa nataka kuishi nao, hakuna njia ningeendelea kuishi na wasichana hao wawili katika nyumba moja,”

“Ilikuwa ngumu kwangu kwa sababu hawakuwa na familia, mama yao hakuwa vizuri, hivyo nilifanya uamuzi mgumu wa kubaki na Morgan na kuwarudisha wasichana wawili kwa kituo cha watoto mayatima,” Aliongeza.

Hata hivyo, Bahati alifichua kwamba miaka kadhaa baadae, alifurahia kukutana na wasichana hao katika muunganik uliojaa hisia tele.

“Tangu wakati huo, ndio nimekuwa nikitoa sapoti yangu mahali ninaweza, kuwalipia karo hapa na pale, lakini hatujawahi jumuika pamoja kujua jinsi wanaendelea. Na leo Purity na Rose wametutembelea na najua wamekuwa wakipitia maisha magumu sana,” Bahati alisema huku akienda kuwakaribisha mabinti hao nyumbani kwake.