“Niliuliza Kanumba mbona ‘Devil Kingdom’ ilibeba maudhui ya kichawi - Pasta aliyeigiza naye

“Kwenye sinema ukimuonyesha mchawi, lazima mwisho umuonyeshe ni namna gani aliteketea kwa sababu tunajua Mungu lazima awe nguvu kumliko shetani. Lakini walisema tutaimaliza hivyo," alieleza.

Muhtasari

• Pasta Myamba alifichua kwamba kwa wakati mmoja, alimkabili Kanumba na kutaka kujua mbona filamu hiyo ilikuwa inatukuza sana uchawi pasi na Mungu kupewa nafasi.

EMMANUEL MYAMBA NA STEVEN KANUMBA.
EMMANUEL MYAMBA NA STEVEN KANUMBA.
Image: HISANI

Emmanuel Myamba, mchungaji kutoka kanisa la House of Victory nchini Tanzania ambaye zamani alikuwa muigizaji na marehemu Steven Kanumba amefunguka kuhusu filamu yenye utata ambayo waliigiza.

Akizungumza na waandishi wa habari, Myamba alifunguka kwamba licha ya kuwa mmoja wa watu walioigiza kwenye filamu tata ya ‘Devil Kingdom’, maudhui ya filamu hiyo yalimpa mashaka sana.

Pasta Myamba alifichua kwamba kwa wakati mmoja, alimkabili Kanumba na kutaka kujua mbona filamu hiyo ilikuwa inatukuza sana uchawi pasi na Mungu kupewa nafasi.

“Kuna filamu ya Devil’s Kingdom tuliyoigiza na Kanumba, ile sinema, hadi mwisho nilikuwa najaribu kujadiliana na wale watu ambao tulikuwa nao. Nikawaambia mbona hii sinema imebeba maudhui mengi sana ya uchawi. Lakini mbona kama Mungu amefinyiliwa sana, na ni vipi tutaifanya mpaka Mungu aonekane mbabe, kwa sababu mwisho wa siku nilikuwa nawaambia lazima ucheze halafu mwisho wa Siku Mungu aonekane kama anashinda,” Myamba alieleza.

Hata hivyo, Myamba alivunjwa moyo sana baada ya Kanumba na wenzake kudinda kubadili script ili kumweka Mungu ndani.

“Kwenye sinema ukimuonyesha mchawi, lazima mwisho umuonyeshe ni namna gani aliteketea kwa sababu tunajua Mungu lazima awe nguvu kumliko shetani. Lakini walisema tutaimaliza hivyo na mimi nilicheza lakini ndani yangu sikuridhika,” aliongeza.

Filamu ya Devil’s Kingdom ilizua nadharia nyingi za uchawi na ushirikina na kwa wakati mmoja ilihusishwa kuwa chanzo cha kifo cha Kanumba, madai ambayo hata hivyo watu wake wa karibu waliyapuuzilia mbali.

Kanumba alifariki mwaka 2012, mwaka mmoja baada ya kuachilia filamu hiyo yenye maudhui tata.