Kijana mmoja alijipatia umaarufu mkubwa wakati wa maandamano ya Gen-z katikati ya mwaka kwa kupinga kwa sauti kubwa kuuzwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Henry Omondi hakuwa mwandamanaji wa kawaida, sauti yake kubwa na shauku yake wakati wa majaribio ya kuandamana hadi JKIA katika lengo la kupinga kuuzwa kwake vilimfanya kuonekana sana na video yake imekuwa ikivuma kwenye mitandao ya kijamii tangu wakati huo.
Kwa sasa yuko mapumzikoni kutoka chuoni ambako anaendelea na kozi ya ufundi na nilimpata ili atueleze kwa ufupi yeye ni nani.
“Kwa majina naitwa Henry Omondi kutoka Siaya. Nilizaliwa 2005, niko na miaka kumi na tisa sasa hivi,” alisema.
Henry alifichua kuwa yeye ni mzaliwa wa kwanza katika familia ya ndugu watano.
Alisema kuwa kwa sasa anasomea kozi ya ufundi wa umeme katika shule ya Ndere Polytechnic iliyoko North Gem, kaunti ya Siaya.
Akizungumzia kisa cha maandamano kilichomfanya avume, kijana huyo alifichua kuwa yeye na waandamanaji wenzake walikuwa wakitarajia kufika uwanja wa JKIA kabla ya kuzuiwa na polisi.
“Hatukifika.
Tulifika Uwanja wa Nyayo. Tulikuwa na nia ya kufika. Vile makarao walifika,
tulitaka kupita barabara ya juu, lakini wakataa. Walikuwa wanapita kwa highway,
na sisi tulikuwa tunapita chini. Sisi tulikuwa tunatembea tu, alafu
wanatuongelesha kwa furaha tunadhani tunaenda kufika. Vile tulifika karibu na
Wilson Hotel, ndio walianza kutupa vitoa machozi. Mimi niliruka Nyayo, watu
walikuwa wanaruka Nyayo. Tulifika kwa boma ingine tukapata watu wanajenga
tukaanza njia ili tukae salama,” Henry alisimulia.
Kijana huyo kutoka Siaya alisema wakati huo alikuwa akiishi katika kituo maarufu cha mabasi jijini kinachojulikana kwa jina Bus Station (BS) na alikuwa akilala hapo.
Alipoulizwa alipataje taarifa za kuuzwa kwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, alisema, “Sikujua, nilikuwa naongea tu."
Hata hivyo alibainisha kuwa ana furaha kuona kwamba hatimaye rais William Ruto alisikia kilio chake kuhusu kukodisha uwanja huo wa ndege na kufuta mkataba na Adani.
Wiki iliyopita, Henry alisafiri hadi Nairobi kwa njia ya anga, tukio ambalo ataishi kukumbuka kwani ilikuwa mara yake ya kwanza kupanda ndege.