Mwendeshaji wa pikipiki maarufu jijini Nairobi Biker Nairobi maarufu kama Brayo amejitolea kumsaidia mwanafunzi mmoja kwa jina Romeo, kupata mhudumu wa pikipiki ambaye atakuwa anampeleka eneo la Rongai kwa ajili ya kushiriki masomo ya ziada wakati huu ambapo shule zimefungwa.
Kwa mujibu wa video aliyochapisha kwenye akaunti zake za mtandaoni mwanafunzi huyo hutembea takribani kilomita 11 kila siku asubuhi na jioni ili kufanikisha ndoto zake masomoni kwa kushiriki masomo ya ziada. Brayo amesema kuwa mwanafunzi huyo hutoka sehemu ya Kibera hadi eneo la Rongai Ngori kufika pahali panapotolewa masomo ya ziada bila malipo.
Katika mazungumzo kati ya Brayo na Romeo, Romeo alikiri kuwa amekuwa akitamani sana kukutana na Brayo kwani yeye ni shabiki mkubwa na mwendeshaji pikipiki huyo kwenye mtandao wa Tik Tok.
“Nimekuwa tu nikikuona nasema mimi nitapatana na wewe lini. Hadi sai nimekuwa nikisema Mungu walahi niokolee ata mimi nipate hivo.” Alisema Romeo.
Romeo alimwambia Brayo kuwa yeye hutembea kila siku kutoka masomo ya ziada eneo la Kona hadi eneo la Rongai karibu na SGR.
Romeo alisema kwamba aliamua kushiriki masomo ya ziada eneo hilo la mbali ili kujaribu kumaliza silabasi ya kidato cha pili kwani haitabiriki ikiwa mwakani ataruhusiwa shuleni kutokana na changamoto za karo.
Mwanafuzni huyo alisema kuwa anaishi na nyanya yake baada ya wazazi wake kuhamia mashambani kutokana na hali ngumu ya maisha. Nyanya ya Romeo ndiye mlezi wa Romeo kwa sasa.
“Wazazi waliniwacha na nyanya wakaenda mashamani, huku waliniwacha na nyanya, yeye ndio mlezi na kila kitu. Yeye ndio mimi hutegemea.” Alisema Romeo.
Kutokana na simulizi hiyo ya Romeo, Biker Nairobi alisema atajaribu kutafuta mtu ambaye atakuwa anamchukua Romeo kila siku na angalau kumfikisha eneo la Lang’ata akielezea matuamaini ya kuwa hawezi kukosekana.
”Wacha nikipata msee mwenye atakuwa anakuja kukuchukua hapa anakufikisha Lang’ata… hakuwezi kosa msee hakuwezi kosa mru akuwe anakufikisha Lang’ata.” Alisema Biker Nairobi.
Hata hivyo, Brayo amewaomba madereva wanaotumia barabara
hiyo kumsaidia Romeo kwa kumbeba kutoka eneo la SGR hadi Lamg’ata.