Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo Joseph Ogidi almaarufu Gidi Gidi na msanii mwenzake wa zamani Julius Owino almaarufu Maji Maji watakuwa miongoni mwa wasanii wakongwe wa Kenya watakaotumbuiza katika tamasha la Jamhuri Day, toleo la Malegendari, mnamo Desemba 12, 2024.
Hafla hiyo iliyoandaliwa na Tume ya Kudumu ya Rais ya Muziki (PPMC) itafanyika katika bustani ya Uhuru.
"Gidi Gidi na Maji Maji watatumbuiza Siku hii ya Jamhuri, Uhuru Gardens, Nairobi" PPMC ilitangaza Jumatatu.
Gidi pia alithibitisha kuhusu tukio hilo kupitia kurasa zake za mitanda ya kijamii.
"Habari ndiyo hiyo," alisema.
Wasanii wengine wakongwe waliopangwa kutumbuiza katika tamasha hilo ni pamoja na; Jaguar, Madtraxx, Mejja, Jua Cali, DNA, VDJ Space, Maroon Commandos, Msanii Music Group, Joyce Bruno, Mercy KeruChuchu, Mr Lenny, Esther Wahome, P-Unit, Joan Nyambura, Rastobelus Iha Mitsanze, Redempter Mumbe, Ruth Mandie, The Bridal Choir, Benjamin Mwiti, Justine Randu, Kairu wa Nyenyenye, na Anita Melo
Irene Kamau, Jillo, Karen Kahato, Mika Kahindi, Were, Benn Prince, Brian Baya, Emmanuel Mwamkemba wa bendi ya Yellow Wagoners pia watatumbuiza.
Mapema mwaka huu, Gidi alifunguka kuhusu uhusiano wake wa sasa na aliyekuwa mwenzake katika kundi la muziki la Gidi Gidi Maji Maji, Julius Owino almaarufu Maji Maji.
Katika mahojiano na KTN Home, mtangazaji huyo wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo aliweka wazi kuwa wao bado ni marafiki wa dhati.
Alifichua kuwa bado huwa wanakutana mara kwa mara, wanajuliana hali na kupata kubadilishana mawazo na kumbukumbu walizounda pamoja.
“Sisi ni marafiki wazuri. Sisi bado ni marafiki wazuri. Wakati mwingine tunakutana, wiki mbili zilizopita tulikuwa naye hapa,” Gidi alisema.
Aliongeza, "Tunashiriki mawazo, tunashiriki kumbukumbu zetu. Wakati mwingine tunakuwa na shinikizo la kurudi studio, lakini nguvu ya kuimba katika umri wetu haipo.
Tena aina ya muziki tuliofanya haidumu kwa muda mrefu. Ni muziki wa msimu, baada ya muda fulani unaenda.”
Mtangazaji huyo mahiri alibainisha kuwa siku hizi yeye na Maji Maji wanajishughulisha na mambo mengi ambayo yanaweza kufanya iwe ngumu kwa wao kurudi kwenye muziki.
Hata hivyo alidokeza kuwa hivi karibuni huenda wakafanya shoo moja kubwa ya mwisho kwa mashabiki wao kusherehekea maisha yao ya muziki yenye mafanikio.
"Tumekuwa tukifikiria kufanya shoo. Hivi karibuni tunapopata wakati au kuamua, au tupate shinikizo kutoka kwa mashabiki, tunaweza kufanya hivyo. Tunaweza kufanya shoo kwa mara ya mwisho,” alisema.