Hivi leo, Januari 4, wanandoa mashuhuri Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel na Esther Musila wanaadhimisha hatua muhimu sana katika uhusiano na ndoa yao.
Wapenzi hao wawili wanaofuatiliwa sana nchini wanasherehekea miaka mitano pamoja na miaka mitatu ya ndoa.
Huku akiadhimisha siku hiyo maalum kupitia mitandao ya kijamii siku ya Jumamosi, Esther alimtambua mumewe kuwa rafiki yake mkubwa zaidi na akabainisha jinsi safari yao pamoja imekuwa nzuri.
"04.01...Siku hii, nilifunga ndoa na rafiki yangu mkubwa na kati ya hadithi zote za mapenzi ulimwenguni, hadithi yetu itakuwa kipenzi changu kila wakati. Hii imekuwa safari nzuri. Mimi bado ni mchumba wako, wewe bado ni bwana harusi wangu,” Esther Musila aliandika kwenye Instagram.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 54 alisherehekea mapenzi yao na kujitakia furaha yeye na mumewe wanapoadhimisha kumbukumbu ya ndoa yao.
“Tukitafakari juu ya safari yetu, kuna mambo matatu ambayo yatadumu daima; IMANI, UPENDO, na TUMAINI. Kubwa kwetu ni UPENDO. MAPENZI YAMESHINDA! Kila siku, ninakupenda zaidi ya siku iliyopita. Unawafanya Bwana & Bibi waonekane rahisi sana, "alisema.
"Heri ya kumbukumbu ya ndoa kwa mpenzi wa maisha yangu na mengi, mengi zaidi yajayo. Mungu wetu akiwa upande wetu. Ushindi umehakikishwa. Kwetu, Kheri ya Kumbukumbu ya ndoa Bwana & Bibi Omwaka,” aliongeza.
Guardian Angel kwa upande wake alibainisha kuwa wanapanga kuboresha uhusiano wao mwaka huu na kuitakia baraka.
"Baraka za siku ya kuzaliwa kwangu. Heri ya kumbukumbu ya miaka 5 kwetu. 2025 ni mwanzo wa msimu wetu mpya wa upendo, afya njema na nguvu,” Guardian Angel alisema.
Guardian Angel na Esther walifanya harusi ya faragha iliyohudhuriwa na marafiki wa karibu na familia mnamo Januari 4, 2022.
Walifunga pingu za maisha baada ya miaka miwili ya kuchumbiana.