
Hafla ya Tuzo za Grammy za mwaka 2025, iliyofanyika katika ukumbi wa Crypto.com Arena, jijini Los Angeles, Marekani ilishuhudia kurejea kwa rapa maarufu Kanye West almaarufu Ye baada ya kutokuwepo kwa muda wa miaka kumi.
Hata hivyo, haikuwa Kanye pekee aliyeshika vichwa vya habari bali pia mke wake, Bianca Censori, ambaye alivaa mavazi yaliyovutia hisia mseto.
Bi Censori alifika kwenye hafla hiyo akiwa amevaa koti kubwa la manyoya meusi, lakini baadaye alilivua na kubaki na rinda lenye kitambaa chepesi sana, kiasi cha kuacha mwili wake wazi kwa kiasi kikubwa.
Watu wengi walistushwa na muonekano wake, huku wengine wakimsifu kwa uthubutu wake wa kisanii na wengine wakikosoa vazi hilo kama lisilofaa kwa tukio la hadhi kubwa kama Grammy.
Mitandao ya kijamii nayo iliwaka moto kwa mijadala. Watu waligawanyika kati ya wale waliotetea mtindo wa Censori wakisema ni ishara ya uhuru wa mavazi na sanaa, na wale waliodai kwamba alivuka mipaka ya maadili ya hadhara.
Wakati huohuo, habari zilivuja kwamba Kanye na Censori huenda hawakuwa wamealikwa rasmi kwenye tuzo hizo na walipewa maelekezo ya kuondoka na walinzi wa usalama.
Baadhi ya ripoti zilidai kuwa uamuzi huo ulitokana na mavazi ya Censori, lakini vyanzo vingine kutoka Marekani vilidai kwamba Kanye aliondoka kwa hiari baada ya kuhudhuria kwa muda mfupi.
Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa Kanye West kuhudhuria tuzo za Grammy tangu 2015, na kurejea kwake kumezua gumzo kubwa.
Tukio hili limechochea mjadala mpana kuhusu mipaka ya mtindo wa mavazi kwenye hafla kubwa na jinsi tasnia ya burudani inavyoendelea kubadilika.
Wakati mjadala ukiendelea, Kanye na Censori wanazidi kuwa gumzo kuu kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.