
Ali Kiba ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii, Instagram akimtaja Sheikh kama aliyekosea kwenye ujumbe wake kuhusu watu wenye utajiri wanavyoendeleza miendendo yao wakati wa kufuturu.
'Mwambie atoe haya katika hili, sheikh wangu amekosea hakuna mipaka katika kufuturisha awe tajiri au maskini, wote wana haki ya kufururishwa. Tafusiri ya kufuturisha ni kumufungulisha aliyefunga hata kwa tende moja au maji, sasa utajuaje kama huyo mtu masikini au tajiri," aliandika Ali Kiba.
"Au kwa unavyosema wanakuja na magari ndio maana wanaonekana matajiri, hata dini inasema tuombe tuwe na neema hapa dunia na kesho akhera kwa maana hiyo watu wasitembee na magari?" aliuliza mwanamziki huyo.
Sheikh huyo ambaye alikumbana na upinzani kutoka kwa Kiba alikuwa ameeleza kwamba hapendezwi na watu wa tabaka la juu wanokwenda msikitini kufuturu kwa magari ya bei ghali na kulisha watu kwa vyakula vingi kisha vinavyobaki vinamwagwa.
"Wasanii na watu maarufu wengi kwenye swala la kufuturisha wanalisha watu vyakula huwa hawafuturishi. sio swala la kutafuta radhi. Ni kutafuta kiki na majina. wewe utakwenda kumfuturisha mtu amekuja na magari makubwa, akifika pale anachukua chakula anakula kidogo na anakiacha kisha vyote vinakwenda kumwagwa," alieleza Sheikh huyo awali.
Sheikh huyo aliendelea na kueleza kwamba lengo la futari ni kuwapa watu wasio na uwezo wala si kuonesha utajiri wako. Na iwapo wanataka kufutisha ni heri wawaite masikini ambao kwao kupata cha kuweka tumboni ni nadra.
"Lengo la futari katika uislamu ni kuwapa watu wasio na uwezo, mtu akitaka kufuturisha waite watu masikini ambao nyama wanakula kwa nadra, na wala chai ya maziwa hawapati. wewe unakwenda kununua kuku kumlisha mtu ambaye kwake amefuga kuku wengi," alieza zaidi Sheikh.
Kiba ni mwanamuziki na mtunzi wa nyimbo wa Tanzania. Yeye ni mmoja wa wanamuziki wenye talanta zaidi Afrika Mashariki na anachukuliwa zaidi kama Mfalme wa Bongo Flava.