
Diamond alikuwa anazungumza haya kwenye mahojiano na mwanahabari baada ya kuanzisha shughuli za ugavi wa misaada kwa baadhi ya wananchi wa Tanzania wakati wa maadhimisho ya Eid ul Fitr 2025.
"Niko na shughuli kule, viongozi tunagawa misaada, mimi nimemaliza nimeachia vijana waendelee na hiyo shughuli sasa," alisema Diamond.
Kiongozi huyo wa lebo ya Wasafi pia aliweka wazi kwamba kama wanadamu wanafaa kusaidiana bila ubaguzi maana kila wakati kila mmoja anamhitaji mwenzake.
"Nimefika hapa kwa sababu ya undugu, unajua lazima uishi na watu vizuri. Hii dunia tunapita. Kuna siku sitakuwepo mambo yangu ndo yatazungumza. Kuna siku nitakuwa na shinda na nitawahitaji kwa hivyo lazima tuishi pamoja kusaidiana na kutegemeana bila kumdharau mtu," Alieleza zaidi.
Mwanamziki huyo maarufu Tanzania na Afrika mashariki ni miongoni mwa wanamziki ambao walijitokeza kusherehekea pamoja na ndugu waisilamu katika maadhimisho ya Eid ul Fitr.
Eid ul Fitr ni sikukuu ya kidini kwa Waislamu wote duniani kote. Eid al-Fitr inaashiria mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani. Eid al Fitr ni thawabu ya Mwenyezi Mungu kwa waumini waliofunga wakati wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Hawa pia ni waumini wanaomshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwapa nafasi na nguvu za kutekeleza amri zake wakati wa mwezi uliobarikiwa wa Ramadhani. Kijadi, Eid al Fitr huadhimishwa kwa siku tatu katika karibu nchi zote za Kiislamu.