Akothee afunguka kwa nini anaishi maisha ya ujana kwa kuchelewa, mbona haumii moyoni anapoachwa

Akothee amefunguka kuhusu jinsi kuwa mama katika umri mdogo kulivyoathiri mtiririko wa maisha yake.

Muhtasari

•Akothee alizungumza kuhusu jinsi alivyotumia siku zake nyingi za ujana kufanya majukumu ya mzazi badala ya kujiburudisha kama vijana wengine.

•Alibainisha kuwa kutumia muda mwingi wa maisha yake kama mama asiye na mchumba  kuliufanya moyo wake kuwa mgumu.

wakifurahia fungate jijini Santorini, Ugiriki.
Akothee na mumewe Denis Shweizer wakifurahia fungate jijini Santorini, Ugiriki.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee amefunguka kuhusu jinsi kuwa mama katika umri mdogo kulivyoathiri mtiririko wa maisha yake.

Katika taarifa ya Jumanne, mama huyo wa watoto watano alizungumza kuhusu jinsi alivyotumia siku zake nyingi za ujana kushughulikia majukumu ya mzazi badala ya kujiburudisha kama vijana wengine wengi katika miaka yao ya 20.

Baada ya kutumia siku zake nyingi za ujana kulea watoto wake, kisha alijitosa katika kutafuta pesa katika miaka yake ya 30 kabla ya kuanza kufurahia maisha katika miaka yake ya 40.

"Samahani ukiniona nikifanya vitu ambavyo nilipaswa kufanya nilipokuwa na miaka ya 20. Kumbuka tu kwamba nilitumia utoto wangu wote kuwa mzazi asiye na kazi wakati wote. Kulea na kuwa baba na mama kwa binti zangu 3. Nilitumia miaka yangu yote ya 30 kutafuta pesa, na sasa katika miaka yangu ya 40, ninachagua tu na kuanza maisha mapya," Akothee alisema kwenye ukurasa wake wa Instagram..

Aliambatanisha taarifa yake na picha ya kumbukumbu yake na watoto wake watatu iliyopigwa wakati alipokuwa bado mama mdogo. Mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alikuwa akitetea hatua yake ya kufurahia maisha yake katika miaka ya 40 na kufanya mambo ambayo kwa kawaida huhusishwa na vijana katika siku zao za ujana.

“Ukiniuliza nina umri gani. Mpendwa, nina umri wa miaka 20 kwa moyo na mwili na akili ya mwanamke mzuri wa miaka 40 na mwenye akili timamu ambaye anajua anachotaka maishani,” aliongeza.

na watoto wake katika siku za nyuma.
Akothee na watoto wake katika siku za nyuma.
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Aidha, mjasiriamali huyo alibainisha kuwa kutumia muda mwingi wa maisha yake kama mama asiye na mchumba  kuliufanya moyo wake kuwa mgumu kiasi kwamba haumii tena kutokana na mahusiano yaliyovunjika.

“Hatuvunjiki moyo tena, kwani wewe una mioyo mingapi? Zile ma character development umepitia bado uko na roho ya kubreakiwa?.Wacha zako wewe, tafuta pesa ndio uelewe hii maneno. Ni njaaaaa ama hisia,” alisema.

Aliongeza, “Heartbreak ya single mothers kama hajazaa na wewe mtoto haipitii wiki tatu . Isipokuwa wewe ndiye breadwinner, uyo atakuwa analilia mkate, kodi na maisha mazuri uliyotoa."

Mama huyo wa watoto watano alifichua  kuwa amewahi kuachwa na watoto watatu huku akiwa hana ajira na elimu ipasavyo. Hata hivyo alibainisha kuwa ni vijana pekee wanaoumia moyo na sio wanawake waliokomaa kama yeye.