Boniface Mwangi azungumza baada ya kupokea mkopo wa Hustler Fund wa Sh1500

"Sasa hii pesa nitapeleka wapi? Unawekeza vipi shilingi 1500?," alihoji.

Muhtasari

•Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, Mwangi alifichua kuwa alichukua mkopo baada ya kufahamu kuhusu hazina hiyo.

•Aidha aliweka wazi kuwa hajali kamwe kuhusu mradi huo.

Mwanaharakati Boniface Mwangi
Image: Hisani

Mwanaharakati maarufu wa kutetea haki za binadamu Boniface Mwangi amedai kuwa hakujua kuhusu Hustler Fund hadi Alhamisi jioni.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Ijumaa, Mwangi alifichua kuwa alichukua mkopo baada ya kufahamu kuhusu hazina hiyo.

Baba huyo wa watoto watatu alisema  alikuwa akijaribu kubaini  kama mradi huo wa serikali unafanya kazi alipopewa mkopo wa Ksh 1500.

"Sasa hii pesa nitapeleka wapi? Nahitaji kuwekeza pesa hizi. Unawekeza vipi shilingi 1500?," Mwangi alihoji.

Mume huyo wa Hellen Njeri alikosoa mradi huo ambao ulizinduliwa Jumatano  na kudai kuwa mfano wa kampeni wenye nia isiyo nzuri.

"Hii ni njia nyingine ya kudanganya wajinga," alisema.

Aidha aliweka wazi kuwa hajali kamwe kuhusu mradi huo.

Mwangi alifichua kuwa siku za hivi majuzi hajakuwa akifuatilia sana yanayoendelea nchini kwani  hajakuwa akitazama ama kusikiliza habari.

Jumla ya Sh1,381,747,777 za Hustler Fund zilikuwa zimetolewa kwa Wakenya kufikia Ijumaa usiku wa manane.

Katika taarifa yake ya Jumamosi, Waziri wa Vyama vya Ushirika na MSMEs Simon Chelugui alisema kuwa wateja 5,191,542 wamejisajili kupata huduma za Hustler Fund.

Jumla ya mikopo ambayo imechukuliwa ni 2,346,675 huku Sh48,526,204 tayari zikiwa zimerejeshwa.

Takwimu zilizotolewa na serikali zinaonyesha kuwa kila sekunde Wakenya wanafanya takriban miamala 223 ya mikopo ya hazina hiyo.

Hazina hiyo imeundwa mahususi kusaidia wafanyabiashara wadogo nchini.

Rais William Ruto alizindua hazina hiyo iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu siku ya Jumatano akitimiza ahadi yake ya kabla ya uchaguzi ya kutenga Sh50 bilioni kwa ajili ya 'mahustlers.'

"Kupitia uzinduzi wa hazina hii, tunasaidia Wakenya wasio na uwezo wa kutosha kwa huduma na bidhaa zinazoitikia biashara zao na vile vile kuwakomboa kutoka kwa mawakala na kuanzisha utamaduni wa kuweka akiba, uwekezaji na usalama wa kijamii," Ruto alisema.

Hustler Fund inaundwa na bidhaa nne – za kibinafsi, biashara ndogo, SME na mikopo ya kuanzia.