Fahamu kwa nini Willy Paul alitupilia mbali azma yake ya kuwania ubunge wa Mathare

Mwimbaji huyo amedokeza kuwa huenda akawania kiti hicho katika siku zijazo.

Muhtasari

•Mwishoni mwa mwaka jana Willy Paul alitangaza mpango wake wa kuwania ubunge wa Mathare kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

•Amesema hakuona haja ya kuendelea na azimio lake kwani tayari ameridhishwa na kazi ambayo Oluoch amekuwa akifanya.

Image: INSTAGRAM// WILLY PAUL

Mwimbaji Willy Paul kwa mara ya kwanza amefichua kwa nini jina lake halikuwa kwenye debe katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 licha ya awali kudokeza mkuwa angewania kiti cha ubunge wa Mathare.

Katika mahojiano na Eve Mungai, Willy aliweka wazi kuwa mbunge wa sasa wa Mathare Antony Olouch ni rafiki yake mkubwa na hakuwa tayari kuanza kulumbana naye.

Alisema hakuona haja ya kuendelea na azimio lake kwani tayari ameridhishwa na kazi ambayo Oluoch amekuwa akifanya tangu achukue usukani wa Mathare

"Mimi ni mkweli na kama wewe ni rafiki yangu mimi huwa mwaminifu kwa urafiki wetu. Huyo ni rafiki yangu, mbona niende kubishana naye saa hii?" Willy alisema.

Hata hivyo alidokeza kuwa huenda akawania kiti hicho katika siku zijazo huku akibainisha kuwa ndoto yake ya kuongoza ingali hai.

"Bado kuna muda. Sikufi saa hii. Ikiwa wakati huo nitakuwa na azma, nitajaribu. Niko na uhakika rafiki yangu Oluoch ataniunga mkono," alisema.

Mwishoni mwa mwaka jana Willy Paul alitangaza mpango wake wa kuwania ubunge wa Mathare kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

"Je, mko tayari Mathare? Tulete mabadiliko hayo," Willy Paul alisema kwenye Instagram.

Aliambatanisha ujumbe wake na picha ya bango lenye sura yake na maandishi "Willy Paul, Mathare MP 2022."

Hata hivyo, hakutangaza chama ambacho angetumia kuwania kiti hicho na hata hakufuata azma hiyo lake zaidi.

Mwimbaji mwenzake Kelvin Kioko almaarufu Bahati aliwania kiti hicho kwa tiketi ya Jubilee ila hakufanikiwa kukitwaa.

Bahati aliibuka wa tatu nyuma ya mbunge wa sasa Antony Oluoch ambaye aliwania kwa tiketi ya wa ODM na Billian Ojiwa wa UDA.

Oluoch alihifadhi kiti chake baada ya kuzoa kura 28,098 katika kinyang’anyiro hicho kilichokuwa na mvutano mkali. Ojiwa ambaye alipata kura 16, 912 hakuridhishwa na matokeo hayo na kuapa kuelekea mahakamani kuyapinga.