Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo Jacob 'Ghost' Mulee amefunguka kuhusu kicheko chake maarufu cha kipekee.
Katika mahojiano na mwandishi Samuel Maina, Ghost alibainisha kuwa kicheko hicho chake ambacho kinapendwa na wengi ni cha kweli na asilia.
Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alisema kwa ujumla yeye ni mtu mwenye furaha na ni mara chache ambapo huwa na hasira.
"Hiki kicheko ni changu halisi. Kawaida yangu mimi ni mtu wa furaha na hivyo ndivyo huwa nacheka. Huwa sina pressure," alisema.
Alifichua kuwa kutokana na madai mengi ya umma anapanga kuweka kicheko hicho kwenye mtandao ili mashabiki waweze kukipata kwa ada kidogo.
Kuhusu uchangamfu wake, alifichua kuwa kila asubuhi huwa anapiga sala kabla ya kutoka nyumbani kuelekea studioni kwa ajili ya shoo yake na Gidi.
"Baada ya maombi, nikija studio huwa sina wasiwasi wowote, najua mambo yatakuwa shwari. Bila maombi inakuwa hujielewi unafanya nini," alisema.
Alidokeza kuwa mashabiki wa Gidi na Ghost asubuhi ndio humpa motisha wa kurauka kila majogoo na kutumbuiza kwa masaa manne.
"Nikijua kwamba watu wananiskiliza, napata motisha. Nikishavaa headphones naingia kweye character nyingine. Inakuwa sasa ni uchangamfu masaa manne, ata kama umekosana na bibi lazima ucheke,"
Ghost alibainisha kuwa kufanya kazi kama mtangazaji mwenza wa Gidi imekuwa ni safari nzuri ya kufarahisha.
Alisema ni mara chache ametofautiana na Gidi kwa miaka kumi na minne ambayo wamefanya kazi pamoja.
"Tumefanya kazi vizuri kwa miaka kumi na nne bila wasiwasi wowote. Hakuna kukorofishana, huwa ni masuala ya kazi, kama kuna tofauti huwa za kikazi na baada ya pale tunatoka tunaenda zetu," alisema.
Mtangazaji na mkufunzi huyo mahiri alilinganisha uhusiano wake wa kikazi na Gidi na ndoa imara.
Hata hivyo, alikiri kuwa kama ndoa nyingine yoyote, hakujakosa changamoto katika 'ndoa' yake na mwenzake. Alibainisha kuwa mara zote Gidi huwa tayari kumrekebisha kila anapokosea kazini.
"Ni ndoa ambayo huwezi kuiacha isipokuwa uamue hivyo. Tumekaa kwa hii ndoa miaka 14. Imekuwa ni changamoto. Gidi ana haiba tofauti na yangu. Lakini nampenda kwa sababu tukifanya naye kazi, unapata saa zingine mimi ni mtu wa mzaha, nikitoka line ananirejesha kama mwalimu mkuu," alisema.
Pia alizungumzia kitengo maarufu kwenye kipindi chao 'Patanisho' na kusema kuwa inawapa furaha nyingi kusaidia watu kurudiana