Harmonize kuwakutanisha mahasidi wakubwa Diamond na Alikiba

Kwa miaka mingi, Diamond na Alikiba wameonyesha wazi uhusiano mbaya kati yao.

Muhtasari

•Diamond na Alikiba ni miongoni mwa wageni wanaotazamiwa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa albamu ya Harmonize jioni ya leo, Mei 25.

•Tukio hilo linaweza kuwa la umuhimu sana kwa tasnia ya bongo fleva ikiwa wote walioalikwa watajitokeza.

Diamond Platnumz, Harmonize, Alikiba
Image: INSTAGRAM

Mahasidi wakuu katika tasnia ya muziki wa bongofleva Diamond Platnumz na Alikiba ni miongoni mwa wageni wanaotazamiwa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa albamu ya Harmonize jioni ya leo, Mei 25.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kondeboy alifichua kuwa wawili hao wamealikwa kwa uzinduzi wa albamu yake ya tano na tayari wamethibitisha kuhudhuria.

Tukio hilo litafanyika katika ukumbi wa Milimani City jijini Dar es Salaam, Tanzania kuanzia saa kumi na moja jioni ya tarehe 25 Mei.

“Simba @diamondplatnumz atakuwepo Mei 25 kwenye uzinduzi wa Albamu ya Harmonize. Viwango vya juu vitaonyeshwa Mei 25 Milimani City City. Harmonize atafanya shoo ya viwango vikubwa,” lilisomeka bango ambalo Harmonize alichapisha Ijumaa.

Pia alishare bango lingine linalothibitisha kuhudhuria kwa bosi wa label ya Kings Music,  Alikiba.

“Mfalme @officialalikiba atakuwepo Mei 25 kwenye uzinduzi wa albamu ya Harmonize,” alisema.

Mastaa wengine wengi wa Tanzania wakiwemo Zuchu, Mboso, Hamisa Mobetto, Ibraah, Irene Uwoya, Rosa Ree, Whozu, Aslay, Jackline Wolper, Wema Sepetu, AY, Rayvanny, Bilnass, Marioo, Ben Pol, Ommy Dimpoz na Mwana FA pia wamealikwa kwa tukio hilo.

Tukio hili linaweza kuwa la umuhimu sana kwa tasnia ya bongo fleva ikiwa wote walioalikwa watajitokeza. Itapendeza kuwaona Alikiba na Diamond wakiwa kwenye hafla moja kwani kwa muda mrefu waimbaji hao wametajwa kuwa na uhusiano mbaya. 

Kondeboy pia hajakuwa na uhusiano mzuri na Diamond Platnumz ambaye alikuwa bosi wake katika lebo ya Wasafi.

Takriban miezi miwili iliyopita, wawili hao walipata fursa adimu ya kuwa kwenye ukumbi mmoja baada ya muda mrefu sana.

Walikutana na hata kusalimiana katika Ikulu ya Tanzania wakati wa sherehe za Iftar ambazo ziliandaliwa na rais Samia Suluhu Hassan.

Mburudishaji Mwijaku alishiriki picha na video za mkutano wao mzuri, na akajipiga kifua kuwa aliwafanya wakutane.

"Nguvu ya mama imeonekana leo, Samia Suluhu Hassan!! Leo nimewakutanisha Diamond Platnumz na Harmonize, nikasema hakuna ninachoweza kushinda!!," Mwijaku alijigamba.

Wawili hao ambao walikuwa wamevalia kanzu nzuri zinazoenda kufanana walionekana kufurahi sana kukutana na wakafanya mazungumzo yasiyosikika.

Alikiba pia alikuwepo katika ikulu wakati wa hafla hiyo lakini haikufahamika ikiwa alipata fursa ya kukutana na kuzunguma na hasidi wake Diamond.