"Huenda nisipate watoto" Mbosso afunguka kuhusu tatizo kubwa la moyo linalomuathiri

Muhtasari

•Mbosso alieleza kuwa hali hiyo inayofanya mwili wake kutetemeka imesababishwa na  kuziba kwa mishipa yake.

•Alifichua  kwamba ni wazazi wake,, baby mamas wake na bosi wake Diamond pekee  ambao wamekuwa wakijua kuhusu hali hiyo.

Staa wa Bongo Mbwana Yusuf Kilungi almaarufu Mbosso amefunguka kuwa anakumbwa na matatizo makubwa ya moyo.

Msanii huyo wa WCB mwenye umri wa miaka 29 amefichua kuwa amekuwa akipambana na hali hiyo kwa kipindi kirefu.

Akiwa kwenye mahojiano na Wasafi Media, Mbosso alieleza kuwa hali hiyo inayofanya mwili wake kutetemeka imesababishwa na  kuziba kwa mishipa yake.

"Nimeambiwa matatizo yangu yanatokana na mishipa yangu ya damu kuzibwa na mafuta. Hali hii haijanipata ukubwani, ni tangu nizaliwe," Mbosso alisema.

Mwanamuziki huyo alifichua kuwa kuna nyakati ambapo hali hiyo  husababisha ganzi mwilini mwake kiasi kwamba anapoteza hisia.

Mbosso alisema ugonjwa huo upo ndani ya familia yake na amekuwa nao tangu kuzaliwa kwake. Alisema kuwa hata hivyo kuna nuru gizani kwani tayari kuna mpango wa hali hiyo kuenda kurekebishwa ughaibuni.

"Nimesisitizwa nifanye mazoezi. Kuna wataalamu pia niliwasiliana nao. Natakiwa nisafiri kwa ajili ya kuenda kupatana nao," Alisema.

Mbosso alisema atasafiri kuenda kutibiwa baada ya kupanga mambo yake nyumbani kwani matibabu yatachukua muda mrefu.

Alifichua kuwa anasaka matibabu kwa kuwa madaktari waliwahi kumwarifu kuwa ugonjwa wake huenda ukamsababishia utasa baada ya kutimiza miaka 30.

"Daktari aliniambia shida yangu huenda ikawa kubwa zaidi  baada ya kufikisha miaka 30. Alisema huenda ikanipelekea nisipate tena watoto nisipofanya matibabu," Alisema.

Mwanamuziki huyo pia aliweka wazi kwamba sio wengi ambao wamekuwa wakifahamu kuhusu ugonjwa wake.

Alifichua  kwamba ni wazazi wake tu, baby mamas wake na bosi wake Diamond Platnumz ambao wamekuwa wakijua kuhusu hali hiyo.