Juliani na aliyekuwa mpenziwe, Brenda Wairimu wamfanyia binti yao karamu ya kifahari

Wawili hao walimsherehekea binti yao Amor Njeri alipokuwa akisherehekea kutimiza miaka 8.

Muhtasari

•Bi Wairimu alimtakia bintiye heri ya siku ya kuzaliwa na kueleza fahari yake ya kuwa mama kwa miaka minane.

•Katika video hiyo, Wairimu alionekana akimsaidia bintiye kukata keki huku akiwaelekeza watoto kumwimbia.

Juliani na aliyekuwa mpenzi wake Brenda Wairimu.
Image: INSTAGRAM//

Siku ya Jumapili, Januari 8, binti ya rapa Juliani na aliyekuwa mpenzi wake Brenda Wairimu aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Wasanii hao wawili walimsherehekea binti yao Amor Njeri alipokuwa akisherehekea kutimiza miaka minane.

"Nimekuwa mama kwa miaka 8, haya ni makubwa, karibu miaka kumi ya uzoefu 😹, niombeni ushauri," alisema kwenye Instagram.

Juliani alichapisha video ya binti yao akikata keki ya siku ya kuzaliwa huku akiwa amezingirwa na watoto wengine kadhaa ambao walikuwa wamekusanyika pamoja kwenye karamu iliyokuwa imeandaliwa kumsherehekea.

Katika video hiyo, Wairimu alionekana akimsaidia bintiye kukata keki huku akiwaelekeza watoto kumwimbia.

"Tuko tayari, tunaimba wimbo gani?" aliwauliza.

Siku chache zilizopita, mwimbaji huyo wa nyimbo za kufoka alishiriki muda na bintiye ambapo alimtazama akionyesha ustadi wake wa kuchora.

"Picasso kwa Castle," Juliani aliandika.

Wazazi wenza hao wawili walitengana takriban miaka minne iliyopita baada ya kuchumbiana kwa takriban miaka minane.

Mwaka jana, Juliani alipokuwa kwenye mahojiano na Standard alifunguka jinsi alivyokutana na mzazi huyo mwenzake.

Alieleza kuwa walikutana mitandaoni baada ya kuona baadhi ya kazi alizokuwa akifanya katika mtaa wa Dandora na akataka kujitolea.

"Nilikutana naye uso kwa uso huko USIU ambako nilikuwa nafanya tour na akaniambia ni shabiki wangu. Tulianza mazungumzo na mambo yakawa sawa. Yeye ni mrembo,"  mwimbaji huyo alisema.

Juliani alisimulia kwamba ingawa alikuwa amepanga kumuoa Wairimu, alifurahi kuwa walikuwa na mtoto mzuri pamoja.

Rapa huyo pia alikuwa akijilaumu kwa kuvunjika kwa uhusiano wao, akisema: “Nilikuwa mtu mwema lakini si mcha Mungu, mahusiano yanafaa yaendelezwe si kwa sababu za ubinafsi... nilikuwa na mambo mengi ambayo hayakuwa mazuri kwake, ukiwa kwenye mahusiano unakuwa sehemu ya huduma, sikufanya hivyo. kuwa na mawazo kama haya."

Kwa sasa, Juliani tayari yuko kwenye ndoa nyingine na aliyekuwa mke wa waziri wa masuala ya kigeni  Alfred Mutua, Lilian Nganga na wawili hao walibarikiwa na mtoto wao wa kwanza pamoja mwaka jana.

Wairimu kwa upande wake amesalia kimya kuhusu maisha yake ya mahusiano.