Mama Dangote ajivunia safari ya mwanawe Diamond, amtia moyo aendelee kupambana

Alibainisha kuwa safari ya muziki ya Diamond imekuwa ndefu lakini akadokeza kuwa bado kuna mengi.

Muhtasari

•Mama Dangote alishiriki picha za kumbukumbu za mwanawe akipokea tuzo katika hafla ya zamani katika siku zake za mwanzo katika tasnia hiyo.

•Mama Dangote alimhakikishia bosi huyo wa WCB kuwa anazidi kumuunga mkono kwa maombi ili apate nguvu ya kuendelea.

amejivunia safari ya muziki ya mwanawe Diamond Platnumz
Mama Dangote amejivunia safari ya muziki ya mwanawe Diamond Platnumz
Image: INSTAGRAM,// MAMA DANGOTE

Mama mzazi wa Diamond Platnumz, Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote ameonyesha kujivunia mafanikio makubwa ambayo msanii huyo ameyapata katika tasnia ya muziki.

Siku ya Jumamosi, Mama Dangote alishiriki picha za kumbukumbu za mwanawe akipokea tuzo katika hafla ya zamani katika siku zake za mwanzo katika tasnia hiyo.

Alibainisha kuwa safari ya muziki ya Diamond imekuwa ndefu lakini akadokeza kuwa bado kuna mengi.

“Maisha kama kioo. Alhamdulillah. Tunamshukuru Mungu kwa hapa tulipofika Naseeb kichwa @diamondplatnumz,” Mama Dangote aliandika kwenye Instagram.

Mama Dangote alimtia moyo mwanae asikate tamaa bali aongeze bidii zaidi ili kupata mafanikio zaidi.

Pia alimhakikishia bosi huyo wa WCB kuwa anazidi kumuunga mkono kwa maombi ili apate nguvu ya kuendelea.

“Japo safari ndefu sana. Lakini mimi Mama yako nazidi kukuombea tuendelee na safari tusichoke Inshalaah,” alimwambia.

Mama Dangote sio tu mama mzazi wa mwimbaji Diamond Platnumz bali pia shabiki wake mkubwa na msukumo maishani.

Wawili hao wanaonekana kuwa na uhusiano wa karibu sana na staa huyo wa bongo fleva hata amemsifia mzazi huyo wake katika nyimbo zake nyingi.

Licha ya kuwa na uhusiano wa karibu sana na mama yake, Diamond Platnumz hata hivyo hamtambui mwanaume anayeaminika kuwa baba yake. Bosi huyo wa WCB na mama yake wanasemekana kumkana Mzee Abdul Juma huku Mama Dangote hata akidai kuwa yeye sio baba mzazi wa mwimbaji huyo.

Mapema mwaka jana, Mzee Abdul alikiri kuwa alipatwa na mshangao mkubwa baada aliyekuwa mkewe, Mama Dangote kumkana kama mzazi mwenza.

Akiwa kwenye mahojiano na Mbengo TV, Mzee Abdul alisema hakutarajia angewahi kumtenga na familia yake na kusisitiza hakukuwa na mpangilio wowote.

Abdul hata hivyo alisema tayari ameyasahau yaliyotokea kati yake na mzazi mwenzake na anaendelea vyema na maisha yake.

"Kuhusu stori ambayo ilitokea na Sanura, mzazi mwenzangu kunitenga  bila mpangilio na kujielewa, nilipatwa na mshangao. Hata hivyo nimesahau, maisha yanaendelea kusema kweli. Bado maisha yanaendelea, namshukuru Mwenyezi Mungu" Mzee Abdul alisema.

Takriban miaka miwili iliyopita, Mama Dangote alishangaza wengi baada ya kudai kuwa Mzee Abdul sio baba mzazi wa Diamond Platnumz  kando na ilivyoaminika ikiaminika kwa miaka mingi.

Kwa sasa Mama Dangote ako kwenye mahusiano na mwanamume anayetambulika kama Uncle Shamte.