"Ndoto imekamilika!" Msanii mpya wa Nandy, Yammi avunja kimya baada ya kutambulishwa

Yammi aliwashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono hadi kufikia pale.

Muhtasari

•Nandy alimtambulisha Yammi kama msanii wa kwanza kuingia kwenye mkataba na The African Princess siku ya Alhamisi.

•Yammi alibainisha kwamba hiyo ni ndoto iliyotimia na akawashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono hadi kufikia pale.

Nandy na msanii wake Yammi
Image: INSTAGRAM// THE AFRICAN PRINCESS

Siku chache tu baada ya kuzindua lebo yake ya muziki ya wasanii wa kike pekee, The African Princess, malkia wa Bongofleva Faustina Charles Mfinanga almaarufu Nandy amemtambulisha msanii wake wa kwanza.

Nandy alimtambulisha Yammi kama msanii wa kwanza kuingia kwenye mkataba na The African Princess siku ya Alhamisi na kumtaka atumie fursa hiyo kujikuza zaidi mwenyewe na kukuza lebo hiyo yake. 

"@yammitz wangu usiniangushe, karibu kwenye ulimwengu wa muziki," aliandika kwenye mtandoao wa Instagram. 

Kupitia ukurasa rasmi wa lebo ya The African Princess, mwimbaji huyo wa kibao  'Ninogeshe' alidokeza kwamba mwimbaji Yami ni mzuri sana katika muziki na ana sauti nzuri ya kumtoa nyoka pangoni.

"Amepikwa na akapikika.Sasa ni muda wa dunia kufurahia kipaji kutoka Tanzania," taarifa ya The African Princess ilisoma.

Akizungumza baada ya tangazo hilo, Yami alishindwa kuficha furaha yake kubwa iliyotokana na hatua hiyo kubwa katika kazi yake ya muziki.

Malkia huyo alibainisha kwamba hiyo ni ndoto iliyotimia na akawashukuru wazazi wake kwa kumuunga mkono hadi kufikia pale.

"Nauacha ujumbe huu kwa dada, rafiki na shujaa wangu @OfficialNandy sio tu kwa kutambua kipaji changu lakini kwa maono ya kuongeza thamani katika muziki wa Tanzania kwa kuinua vipaji vya watoto wa kike, mimi ni dhahabu lakini bila kusafishwa ningebaki kuwa jiwe tu, Leo hii mimi ni msanii wa kwanza kuwa chini ya @The_african_princess_label,"  Yammi alimwandikia bosi wake mpya.

Pia alitoa shukrani za dhati kwa kampuni inayohusika katika kusambaza muziki wake kwa kuchangia katika mafanikio yake.

"Kwako wewe shabiki yangu mpya kabla ya yote nasema Asante kwa kuniamini, utakapo liskia jina langu “YAMMI” tambua Umeona binti mwenye Ndoto ya kuwa bora katika mziki, na utakapo isikia sauti yangu tambua ni sauti ya “binti wa Malkia” Naianza safari hii nakuomba uwe nami leo, Naomba tuwe pamoja na ahadi yangu nitakuwa sababu yako ya kuupenda mziki❤️," aliwaambia mashabiki wake.

Nandy alizindua lebo ya The African Princess siku ya Jumatatu, Januari 16 na akatangaza kwamba itakuwa ya wasanii wa kike pekee.