Nilianza ukufunzi nikiwa na umri wa miaka 13- Ghost Mulee azungumza

Ghost alifichua kuwa alianza kukimbiza ndoto yake ya kuwa kocha akiwa shule ya upili.

Muhtasari

•Ghost amefichua kwamba kuwa kocha wa timu ya taifa ya kandanda ilikuwa ndoto yake kuu tangu utotoni.

•Alieleza fahari yake kwa kuweza kuiwakilisha Kenya kama kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka kwa mara tatu.

Jacob 'Ghost' Mulee

Mtangazaji wa kipindi cha Gidi na Ghost asubuhi kwenye Radio Jambo, Jacob 'Ghost' Mulee amefichua kwamba kuwa kocha wa timu ya taifa ya kandanda ilikuwa ndoto yake kuu tangu utotoni.

Katika mahojiano na mwandishi Samuel Maina, Ghost alifichua kuwa alianza kukimbiza ndoto yake ya kuwa kocha akiwa katika shule ya upili.

"Kambumbu imekuwa ndiyo ilikuwa maisha yangu. Nilitaka kuwa kocha wa timu ya taifa. Mungu alinibariki nikawa kocha wa taifa, ilikuwa ni ndoto yangu tangu nikiwa na umri wa miaka 13, nafikiri nilikuwa katika kidato cha pili," alisema.

Kocha huyo wa zamani wa Harambee Stars alifichua kuwa alifanikiwa kutwaa taji lake la kwanza kama kocha akiwa katika kidato cha tatu.

Ghost alieleza fahari yake kwa kuweza kuiwakilisha Kenya kama kocha mkuu wa timu ya taifa ya soka kwa mara tatu.

"Matarajio yangu yalikuwa kuwa kocha hasa wa timu ya taifa, na Mungu alinifaidi, nimekuwa kocha mara tatu. Nimeitwa, nikafutwa, nikaitwa tena na nikafutwa, mpaka siku ya mwisho. Nashukuru," alisema.

Mtangazaji huyo wa kipindi cha asubuhi hata hivyo alisema kuwa mara ya mwisho alihudumu kama kocha wa taifa ilikuwa ndio mwisho wake na akaweka wazi kuwa hatazamii kuchukua nafasi hiyo tena.

Alifichua kuwa kwa sasa anajihusisha na shughuli zingine zinazohusiana na kandanda ikiwa ni pamoja na kusimamia shule yake ya Liberty Sports Academy ambayo ilimtoa mshambulizi Michael Olunga.

"Mimi pia ni mwalimu wa wakufunzi hapa nchini. Pia mimi ni mwanachama wa Makocha hapa nchini, tuna mfumo unaojulikana kama KEFOCA. Kwa umbali, pia natangaza mambo ya kambumbu," alisema.

Aidha, Ghost alimpongeza waziri mpya wa michezo Ababu Namwamba kwa mabadiliko ambayo amefanikisha katika kipindi kifupi ambacho amekuwa ofisini. Alisema kuwa ana imani kubwa na Mhe Ababu.