Nilitamani nigombane na Diamond ili niwe na Zuchu- Rayvanny akiri

Msanii huyo wa zamani wa WCB alidokeza kuvunjika kwa mahusiano yake na Paula Kajala.

Muhtasari

•Staa huyo aliendelea kukiri kummezea mate malkia wa Bongo Nandy kabla yake kufunga ndoa na Bilnass.

•Pia alikiri kutaka kuanzisha vita  na aliyekuwa bosi wake Diamond ili amyakue  anayedaiwa kuwa mpenzi wake Zuchu.

Rayvanny na Zuchu
Image: HISANI

Usiku wa Jumamosi staa wa Bongo Rayvanny alitumbuiza katika tamasha la Fiesta 2022 huko mjini Sumbawanga, Tanzania.

Katika tamasha hilo msanii huyo wa zamani wa WCB alitumbuiza nyimbo zake kadhaa na za wasanii wengine.

Wakati akitumbuiza wimbo wake 'Naogopa', Rayvanny aliongeza mistari kadhaa iliyosikika kama ujumbe wa kukiri. Bosi huyo wa Next Level Music  alidokeza kusambaratika kwa mahusiano yake na Paula Kajala.

"Mapenzi yasikuchanganye nakwambia, usije ukapata bila kama Dulla. Mapenzi usije kufananisha,  kama  vile chakula. Nilinyosha moyo Karula, nikaachana na Paula..." aliimba.

Staa huyo aliendelea kukiri kummezea mate malkia wa Bongo Nandy kabla yake kufunga ndoa na Bilnass.

Pia alikiri kutaka kuanzisha vita  na aliyekuwa bosi wake Diamond ili amyakue  anayedaiwa kuwa mpenzi wake Zuchu.

"Mapenzi yanafanya nichanganyikiwe, niwe na uchu. Nilitamani nigombane na Simba, niende kwa Zuchu," aliimba Rayvanny.

Haya yanajiri wakati mpenzi wa sasa wa mwimbaji huyo bado ni kitendawili. Kumekuwa na tetesi kuwa mahusiano yake na Paula yaligonga ukuta na pia imedaiwa kuwa bado yuko pamoja na baby mama wake Fahyma.

Takriban miezi miwili iliyopita Rayvanny aliondoka WCB baada ya kuwa pale kwa miaka sita. Maelezo machache tu yalitolewa kuhusu sababu zake kuondoka ila ilisemekana kuwa alitaka kuangazia lebo yake mwenyewe.

Katika taarifa yake ya kutangaza kuondoka, aliushukuru uongozi mzima wa Wasafi ukiongozwa na Diamondna kubainisha kuwa alifurahia kipindi chake pale.

“Miaka 6 sasa tangu tumeanza kufanya kazi pamoja na hii timu yangu, familia yangu, WCB Wasafi. Upendo, umoja vimekuwa nguzo kubwa saba kama timu. Mengi nimejifunza lakini pia mengi tumefanikisha tukiwa pamoja,” alisema kupitia video.

Msanii huyo alimshukuru Diamond zaidi kwa kumuaminia miongoni mwa wasanii wengi na kumpa mkataba ndani ya  WCB  ambapo ndipo alipoboresha talanta yake na kujizolea mashabiki wengi alio nao.

Diamond alionekana kumpa msanii huyo wake wa zamani kibali cha kuondoka na kumtakia mema katika taaluma yake.