"Nipo single!" Tanasha Donna atangaza sifa anazozingatia kwa mwanaume

Tanasha alibainisha kuwa hazingatii sura ya mwanaume wala utajiri wake anapotafuta mchumba.

Muhtasari

•Tanasha Donna alidokeza kuwa yuko tayari kumpa mwanaume mwingine nafasi katika moyo wake.

•Pia aliweka wazi kuwa mwanaume anayetazamia kuchumbiana naye ni sharti awe na bidii na Mcha Mungu.

Image: INSTAGRAM// TANASHA DONNA

Mwimbaji na mwanamitindo maarufu wa Kenya ,Tanasha Donna, ameweka wazi kuwa hana yeyote mchumba kwa sasa.

Katika mahojiano ya hivi majuzi, mpenzi huyo wa zamani wa Diamond Platnumz pia alidokeza kuwa yuko tayari kumpa mwanaume mwingine nafasi katika moyo wake.

"Nipo single! Labda kuna mtu ambaye anaweza kuwa mpenzi anayefuata, inaweza kuwa," Tanasha alisema katika mahojiano ya YouTube na Mpasho.

Mama huyo wa mvulana mmoja alibainisha kuwa hazingatii  sura ya mwanaume wala utajiri wake anapotafuta mchumba.

Alifichua kuwa jambo la msingi analozingatia kwa mwanamume  anayekusudia kuchumbiana naye ni tabia yake.

"Tabia ni muhimu sana kwangu. Ni ufunguo wa kila kitu maishani kwa sasa kando na Mungu, mimi ni muumini pia," Alisema.

Tanasha pia alidokeza kuwa mwanaume anayetazamia kuchumbiana naye ni sharti awe mwenye bidii na Mcha Mungu.

"Lazima awe na bidii, lazima awe muumini. Mtu ambaye anaweka Mungu mbele, ni lazima umpende Mungu zaidi ya unavyonipenda. Ni lazima uwe unafanya kitu kwa sababu pia mimi najaribu kujifanyia kitu. Kama hutengenezi kitu kwa ajili yako nitaona kama wewe ni mzembe ama huweki bidii ya kutosha. Sio lazima uwe tajiri lakini lazima uwe unafanya kazi kwa bidii," Alisema Tanasha.

Pia alisema ni sharti mwanaume ambaye anamdai awe na maono kadhaa anayolenga kutimiza maishani.

Takriban miaka miwili iliyopita, Tanasha alitengana na staa wa Bongo Diamond Platnumz baada ya kuchumbiana naye kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Wawili hao walikuwa kwenye mahusiano wazi kati ya 2018 na April 2020 wakati ambapo waliamua kuenda njia tofauti.

Kwa sasa wanashirikiana katika malezi ya mtoto wao, Naseeb Juniour, ambaye alizaliwa mwezi Oktoba 2019.